LUKUMAY AKONGA NYOYO ZA WANANCHI ARUMERU MAGHARIBI, WAZEE WA KIMASAI WAMVALISHA MAVAZI YA HESHIMA ,WAMWOMBEA AONGOZE ZAIDI YA MIAKA MITANO

LUKUMAY AKONGA NYOYO ZA WANANCHI ARUMERU MAGHARIBI, WAZEE WA KIMASAI WAMVALISHA  MAVAZI YA HESHIMA ,WAMWOMBEA AONGOZE ZAIDI YA MIAKA MITANO

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU


Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameendelea kujijengea imani kubwa kwa wananchi baada ya kupokelewa kwa shangwe na heshima kubwa katika Kata za Mwandeti na Musa, huku wazee wa kimila wa Kimasai wakimwombea kwa dua maalumu ili aendelee kupewa afya, hekima na nafasi ya kuwatumikia wananchi kwa kipindi kirefu zaidi kutokana na juhudi zake za kutetea maslahi yao.

Katika ziara yake ya siku ya pili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, Dkt. Lukumay alipokelewa kwa bashasha huku wa zee wa kimil wakimvisha mavazi ya heshima ya Kimasai katika mikutano ya hadhara iliyofanyika Kijiji cha Losikito, Kata ya Mwandeti na Kijiji cha Neng'ung'u, Kata ya Musa.

Wananchi waliinuka kwa shangwe na kumvika mbunge huyo mavazi ya kimila pamoja na kumpatia zawadi mbalimbali kama ishara ya kuthamini kazi anayoifanya ya kuwasemea bungeni na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo hilo.

Wakizungumza mbele ya mamia ya wananchi, wazee wa kimila walimwombea kwa lugha ya Kimasai wakisema anatakiwa kuendelea kupewa nguvu za kuwaongoza wananchi na kutetea maendeleo yao, wakieleza kuwa sauti yake imekuwa msaada mkubwa katika kufikisha kero za Arumeru Magharibi kwenye Serikali.

Wananchi hao walieleza kuwa tangu achaguliwe kuwa mbunge, Dkt. Lukumay amekuwa mstari wa mbele kupaza sauti kuhusu changamoto za maji, barabara, elimu na huduma nyingine muhimu, huku baadhi ya changamoto hizo zikianza kupatiwa ufumbuzi na Serikali.

Pamoja na kumpongeza, wananchi walimuomba kuendelea kuwa sauti yao bungeni ili kuhakikisha changamoto zilizobaki, hususan upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Katika ziara hiyo, Dkt. Lukumay aliambatana na wataalamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru ambao walitoa ufafanuzi na majibu kuhusu hoja zilizotolewa na wananchi, huku tatizo la maji likitajwa kuwa kero kubwa zaidi ikifuatiwa na ubovu wa barabara.

Akizungumza katika mikutano hiyo, Dkt. Lukumay aliwahakikishia wananchi kuwa ataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kwamba hoja zote ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi ataziwasilisha katika kikao kijacho cha Bunge kinachotarajiwa kuanza mwezi Agosti.

Alisema dhamira yake ni kuona kila kata ya Arumeru Magharibi inanufaika na maendeleo bila kujali umbali wake, huku akisisitiza kuwa ataendelea kufanya ziara za mara kwa mara kusikiliza wananchi ana kwa ana badala ya kusubiri taarifa kufikishwa ofisini kwake.

Ziara hiyo inaendelea baada ya Dkt. Lukumay kutembelea Kata za Oldonyowasi na Oldonyosambu, ambako pia alisikiliza kero za wananchi na kuahidi kushughulikia zile zinazoweza kutatuliwa kwa ngazi ya halmashauri na kuzipeleka bungeni zile zinazohitaji maamuzi ya Serikali Kuu.





Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم