FIDIA YA MRADI WA MAGADI SODA YAZUA MASWALI MONDULI, MBUNGE AINGILIA KATI
Na Joseph Ngilisho | MONDULI
WAKATI Serikali ikiendelea na utekelezaji wa Mradi wa Kimkakati wa Magadi Soda wa Engaruka wilayani Monduli, baadhi ya wananchi wameibua malalamiko kuhusu ucheleweshaji wa malipo ya fidia na matumizi ya maeneo ya malisho, hali iliyomlazimu Mbunge wa Monduli, Isack Joseph, kuahidi kuisimamia Serikali kuhakikisha haki ya wananchi inalindwa.
Hoja hizo ziliibuliwa wakati wa ziara ya mbunge huyo ya kukagua miradi ya maendeleo, kuwashukuru wapiga kura na kusikiliza kero za wananchi katika maeneo yanayonufaika na mradi huo mkubwa wa kimkakati unaotekelezwa na Serikali kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Akizungumza mbele ya wananchi, Mbunge Isack Joseph alisema hataruhusu wananchi wanaostahili fidia kuachwa nyuma na kuahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa malipo hayo hadi kila mwenye haki atakapolipwa.
Alisema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha miradi ya kimkakati inatekelezwa sambamba na kulinda maslahi ya wananchi wanaopisha maendeleo, akisisitiza kuwa fidia kwa wanaostahili inapaswa kutolewa kwa wakati ili kuondoa malalamiko na migogoro isiyo ya lazima.
Kwa mujibu wa wataalamu wa ardhi wanaosimamia mradi huo, jumla ya wananchi 559 wanatarajiwa kunufaika na fidia inayohusiana na utekelezaji wa mradi huo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu hatua ya malipo, Mtaalamu wa Ardhi, Waziri Sonyo, alisema Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 14 kwa ajili ya utekelezaji wa fidia na shughuli nyingine zinazohusiana na mradi huo.
Alisema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 5.4 zilitengwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi 519, huku shilingi bilioni 8.6 zikielekezwa katika maendeleo ya vijiji vinne vinavyohusika na mradi huo.
Sonyo alisema wananchi wengi tayari wamekwishalipwa fidia zao, huku kiasi cha shilingi milioni 241 pekee kikiwa bado hakijakamilika kulipwa kutokana na taratibu mbalimbali zinazoendelea kukamilishwa.
Mradi wa Kimkakati wa Magadi Soda wa Engaruka unahusisha vijiji vya Mbaash, Engaruka Chini, Idonyonado na Irerendeni, na unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa magadi soda.
Pia kuongeza thamani ya rasilimali za madini, kuchochea maendeleo ya viwanda, kufungua fursa za ajira na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Hata hivyo, wananchi wameendelea kusisitiza kuwa pamoja na kuunga mkono utekelezaji wa mradi huo, wanahitaji kuona ahadi za fidia zikitekelezwa kwa wakati ili maendeleo yanayoletwa na mradi huo yaende sambamba na kulinda haki na ustawi wa jamii zinazouzunguka.
Ends...










Post a Comment