SAMIA APINGA KILA MRADI KUITWA JINA LAKE, ATAKA WAHERI WA SHERIA WAENZIWE
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa sekta ya sheria kuacha utaratibu wa kuipa kila programu, mradi au taasisi mpya jina lake, akisema hatua hiyo imeanza kujirudia kupita kiasi na kupoteza upekee wa mipango hiyo.
"Kwenye sekta ya sheria tayari tuna Mama Samia Legal Aid Campaign. Kwa tukisema Mama Samia Center of Excellence, Mama Samia... zinakwenda kuwa monotona. Nadhani tubakie na lile moja," alisema.
Rais Samia alipendekeza Kituo cha Umahiri katika Sekta ya Sheria (Center of Excellence) kipewe jina la mwanasheria mashuhuri aliyetoa mchango mkubwa katika taaluma hiyo badala ya kutumia jina lake.
"Hii Center of Excellence ya Sheria tuitafutie mwanasheria mahiri tumpe jina lake. Wenyewe mtaamua kama mtampa jaji wenu au nani, lakini mtaamua," alisema.
Aidha, alikataa pendekezo la mpango wa mafunzo kuitwa Mama Samia Training Programme, akieleza kuwa tayari Wizara ya Elimu ina Mama Samia Scholarship, hivyo majina hayo yangejirudia na kuondoa utofauti.
"Kwa upande wa mpango wa mafunzo tayari Wizara ya Elimu ilishawawahi. Kule kuna Mama Samia Scholarship. Hasa ukiuita tena mpango wa mafunzo wa Mama Samia, zinajirudia rudia, haipendezi," alisema.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema hafurahishwi na mwenendo wa kila sekta kutaka kutumia jina lake, akisisitiza kuwa Tanzania ina viongozi na wataalamu wengi waliotoa mchango mkubwa unaostahili kutambuliwa kwa kupewa heshima hiyo.
"Sasa Mama Samia huyu akiwa kila pahali, inachosha, haipendezi. Kwa hiyo taasisi nyingine wapeni majina. Tupo wengi, tunafanya mazuri mengi," alisema.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia aliwataka mawakili wa serikali na maafisa sheria kuendelea kuijenga sekta ya sheria kwa kuzingatia maadili, ubunifu na weledi.
"Chama hiki cha Mawakili wa Serikali na Maafisa wa Sheria Tanzania kinapaswa kuwa chombo cha kujenga uelewa, maadili, nidhamu, ubunifu na mustakabali wa sekta ya sheria nchini," alisema.
Ends.



Post a Comment