MAAFISA AFYA ARUSHA WAHUKUMIWA KWA KOSA LA KUOMBA NA KUPOKEA RUSHWA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MAAFISA wawili wa Afya wa Kata ya Terati katika Halmashauri ya Jiji la Arusha wamehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Arusha baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa ya Shilingi milioni moja kutoka kwa meneja wa kiwanda cha Mbundimbundi kinachotengeneza pombe kali.
Waliohukumiwa ni Dickson Chinyuka Ndumbalo na Keneth Tamzi Twinzi, ambao walikutwa na hatia ya makosa mawili ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya mwaka 2023.
Hukumu hiyo ilisomwa Mei 28, 2026 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Regina Oiyer, baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote katika shauri la jinai namba CC 17569/2025.
Mahakama iliwahukumu washtakiwa hao kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Shilingi 500,000 kwa kila kosa. Hata hivyo, washtakiwa wote walichagua kulipa faini iliyotolewa na mahakama.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, maafisa hao waliomba na kupokea rushwa ya Shilingi milioni moja kutoka kwa Meneja wa Kiwanda cha Mbunumbundi kwa lengo la kutomchukulia hatua za kisheria kuhusiana na tuhuma za uchakavu wa magari ya kiwanda hicho.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha Julai 18, 2025 na kusikilizwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Arusha. Upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Wakili Msomi Melvin Richard na Wakili Msomi Halima Saidi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngajilo, alisema taasisi hiyo imefanikiwa kushinda shauri hilo na kuonesha dhamira ya serikali ya kuendelea kupambana na vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alisema TAKUKURU itaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha vitendo vya rushwa vinatokomezwa na wananchi wanapata huduma kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Ngajilo pia alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu viashiria vya rushwa kwa mamlaka husika na kujitokeza kutoa ushahidi pale watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani ili kusaidia vyombo vya sheria kutenda haki.
Ends..

إرسال تعليق