WANAFUNZI SABA WAZUILIWA SIKU 30 KUFUATIA MOTO ULIOUA WANAFUNZI 16 KENYA
Na Arushadigital | NAIROBI
Mahakama ya Naivasha, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya, imeamuru wanafunzi saba wa kike wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Utumishi Girls Academy kuzuiliwa kwa siku 30 ili kupisha uchunguzi wa kina kuhusu tukio la moto lililoteketeza bweni la shule hiyo wiki iliyopita na kusababisha vifo vya wanafunzi 16.
Uamuzi huo umetolewa wakati uchunguzi ukiendelea, huku wanafunzi hao wakiwa bado hawajasomewa mashtaka rasmi kutokana na kukamilika kwa taratibu za uchunguzi. Kesi hiyo imevutia hisia kubwa za umma, ambapo ndugu, jamaa na marafiki wa washukiwa pamoja na familia za waathiriwa walifurika katika viunga vya mahakama kufuatilia mwenendo wa shauri hilo.
Washukiwa hao walikamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) baada ya uchunguzi wa awali kuonyesha uwezekano wa kuhusika kwa baadhi yao katika mkasa huo wa kutisha. Moto huo, mbali na kusababisha vifo vya wanafunzi 16, pia uliwaacha wengine kadhaa wakiwa na majeraha ya viwango mbalimbali.
Polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini mazingira kamili ya tukio hilo, huku wakichunguza uwezekano wa kufunguliwa kwa mashtaka ya mauaji na uchomaji moto kwa makusudi dhidi ya wahusika watakaobainika.
Kwa mujibu wa taarifa za wachunguzi, baadhi ya wanafunzi waliohojiwa walieleza kuwepo kwa malalamiko yaliyohusiana na mabadiliko ya ratiba ya mitihani, michango ya shughuli za kitamaduni shuleni na kile kilichoelezwa kuwa ushawishi kutoka kwa wanafunzi wa shule jirani waliokuwa wakifanya maandamano.
Taarifa za DCI zinaeleza kuwa mpango wa kuchoma bweni hilo ulidaiwa kujadiliwa majira ya saa tatu usiku kabla ya kutekelezwa saa chache baadaye. Uchunguzi pia unategemea vielelezo mbalimbali, ikiwemo picha za kamera za usalama (CCTV) ambazo zinaripotiwa kurekodi matukio muhimu kabla na wakati wa kutokea kwa moto huo.
Katika hatua ya kuhakikisha haki na ustawi wa watoto unazingatiwa wakati wa uchunguzi, maafisa wa Kitengo cha Ulinzi wa Watoto cha DCI pamoja na wataalamu wa ushauri nasaha walishiriki katika mahojiano yaliyofanyika katika Kituo cha Polisi cha Gilgil.
Wachunguzi wa Kitengo cha Mauaji wameeleza kuwa bado wanatafuta watu wengine wanaoweza kuwa walihusika katika tukio hilo, hasa baada ya kubainika kuwa mafuta ya taa yalitumika kuanzisha moto huo. Ugunduzi huo umeibua maswali kuhusu chanzo na namna mafuta hayo yalivyoweza kuingizwa na kutumiwa ndani ya mazingira ya shule.
Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea huku mamlaka zikiahidi kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuhusika na mkasa huo ulioitikisa Kenya na kuacha simanzi kwa familia nyingi.

إرسال تعليق