UBOJA YAWEKEZA ZAIDI YA SH. MILIONI 370 KWENYE MRADI WA PIKIPIKI,YAZINDUA MFUMO WA MALIPO WA KIDIGITAL
Na Joseph Ngilisho|ARUSHA
Akizungumza baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za umoja kwa kipindi cha mwaka mmoja mbele ya Halmashauri Kuu ya Wilaya, Katibu wa UBOJA, Richard Maghembe, alisema uongozi umejikita katika kutekeleza miradi yenye matokeo yanayowanufaisha wanachama badala ya kutoa ahadi zisizotekelezeka.
Alisema taarifa hiyo ilihusu utekelezaji wa shughuli za umoja kuanzia Juni 2025 hadi Juni 2026 na imepokelewa vizuri na wajumbe baada ya kuonyesha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho.
Maghembe alisema Septemba mwaka jana UBOJA ilipokea Sh milioni 30 zilizorejeshwa kupitia TAKUKURU, fedha ambazo ziliamuliwa kuwekezwa katika mradi wa pikipiki ili kuongeza kipato cha umoja na kuwainua wanachama kiuchumi.
Alisema mradi huo ulianza kwa kununua pikipiki kumi na kukopeshwa nyingine 10 kwa wanachama, lakini kutokana na urejeshaji mzuri wa mikopo, kampuni inayoshirikiana na UBOJA iliendelea kuongeza idadi ya pikipiki hadi kufikia 124.
Kwa mujibu wa Maghembe, thamani ya mradi huo kwa sasa imefikia zaidi ya Sh milioni 372 na unatarajiwa kuingiza faida ya zaidi ya Sh milioni 60.7 baada ya kukamilika.
"Wanachama wanahitaji matokeo, si maneno. Mafanikio haya yametokana na uaminifu, uwajibikaji na kujitolea kwa viongozi katika kusimamia rasilimali za umoja," alisema.
Katika hatua nyingine, UBOJA imezindua mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao (online) utakaowawezesha wanachama kulipa ada, kufuatilia salio la mikopo na kuona taarifa zao za mikataba popote walipo bila kulazimika kufika ofisini.
Alisema mfumo huo utaongeza uwazi katika utoaji wa huduma, kupunguza matumizi ya makaratasi, kuondoa upotevu wa nyaraka na kudhibiti udanganyifu wa taarifa.
Maghembe alisema kwa sasa UBOJA ina wanachama 9553 waliosajiliwa katika mfumo wake na inalenga kuongeza idadi hiyo sambamba na kupanua miradi ya kiuchumi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Aliongeza kuwa moja ya malengo makubwa ya umoja huo ni kuwaondoa waendesha bodaboda wasiopungua 1,000 kwenye mikataba kandamizi kwa kuwaunganisha na fursa za mikopo nafuu na mikataba yenye maslahi kwa wanachama.
Akizungumzia usalama barabarani, alisema UBOJA inaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa elimu ya usalama barabarani pamoja na kuhakikisha wanachama wanaopata pikipiki kupitia miradi ya umoja wanakuwa na leseni halali na mafunzo ya uendeshaji salama ili kupunguza ajali zinazohusisha bodaboda.
Ends...



Post a Comment