TANFORM YAWAPA BODABODA FURSA YA KUMILIKI MAGODORO KWA MKOPO, YATAKIWA KUIMARISHA AFYA NA UZALISHAJI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
KAMPUNI ya kutengeneza magodoro na bidhaa za kulalia ya Tanform imezindua mpango maalumu wa kuwawezesha waendesha bodaboda na maafisa usafirishaji nchini kumiliki magodoro bora kwa mfumo wa mkopo wa miezi mitatu, ikiwa ni sehemu ya kuboresha ustawi wao na kuongeza ufanisi katika kazi zao za kila siku.
Akizungumza jijini Arusha juni 30,2026 wakati wa utoa wa taarifa ya maendeleo ya UBOJA katika kipindi cha mwaka mmoja , Afisa Mauzo wa Tanform, Daniel Philipo Marko, alisema kampuni hiyo imekuwa mshirika wa karibu wa umoja huo kwa miaka kadhaa na sasa imekuja na suluhisho litakalowarahisishia wanachama kupata magodoro bora bila kulazimika kulipa fedha zote kwa wakati mmoja.
Alisema mpango huo unalenga kuhakikisha madereva wa bodaboda na maafisa usafirishaji wanapata sehemu salama na yenye ubora wa kupumzikia, jambo ambalo litawawezesha kuamka wakiwa na nguvu na kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi.
"Kwa kupitia viongozi wa vikundi vyao, wanachama wataweza kujisajili na kupata magodoro kwa mkopo wa miezi mitatu. Tunaamini kulala vizuri si anasa bali ni hitaji muhimu la maisha. Mtu anayepumzika vizuri ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kuchangia maendeleo ya taifa," alisema Daniel.
Alieleza kuwa Tanform ilianza kushirikiana na waendesha bodaboda miaka iliyopita kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji, ingawa mpango huo ulisimama kwa muda kutokana na changamoto zilizojitokeza. Hata hivyo, sasa umerejea kwa nguvu zaidi ukiwa na mfumo wa kisasa wa kufuatilia malipo unaorahisisha viongozi wa vikundi kusimamia marejesho ya wanachama wao.
Kwa mujibu wa Daniel, mkoa wa Arusha pekee una zaidi ya waendesha bodaboda 40,000, idadi inayoonesha ukubwa wa soko na umuhimu wa kuwafikia kundi hilo. Alisema baada ya Arusha, mpango huo utapanuliwa katika mikoa mingine nchini ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza na Kanda ya Ziwa pamoja na maeneo mengine.
"Mpango huu hauishii Arusha. Tunataka kuwafikia maafisa usafirishaji na waendesha bodaboda nchi nzima kwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kulala kwenye godoro bora na kuwapa fursa ya kumiliki bidhaa zetu kwa utaratibu rahisi wa malipo," aliongeza.
Daniel alisema Tanform inaendelea kuthibitisha ubora wa bidhaa zake baada ya kutwaa tuzo nchini Kenya mapema mwaka huu, akibainisha kuwa magodoro ya kampuni hiyo yanadumu kwa zaidi ya miaka 25.
"Watanzania walitupigia kura na tukashinda tuzo Nairobi. Ubora wa bidhaa zetu unaendelea kuaminiwa. Tuna msemo kwamba godoro la Tanform linaweza kununuliwa na babu na likatumika hadi kwa mjukuu," alisema.
Mbali na magodoro, Daniel alisema Tanform huzalisha bidhaa mbalimbali za chumbani ikiwemo vitanda, mito, mashuka, maduveti, mashuka ya kufunika magodoro na vifaa vingine vya kulalia.
Aliwataka wananchi, vikundi vya vijana na wafanyabiashara kutumia fursa zinazotolewa na kampuni hiyo, ikiwemo kuwa mawakala wa bidhaa za Tanform, ili kujiongezea kipato huku wakisambaza bidhaa bora kwa Watanzania.
Ends..

Post a Comment