WAZIRI NDEJEMBI AAGIZA MRADI WA HALE UKAMILIKE JULAI 31, AKATAA NYONGEZA YA MUDA
Na Hadija Bagasha-TANGA
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, alipokagua maendeleo ya mradi huo, ambapo alisema serikali haijaridhishwa na kasi ya utekelezaji kutokana na mradi kuchelewa kukamilika kwa miezi 10 tofauti na ratiba ya awali.
"Mradi huu uko nyuma ya ratiba. Leo tumemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi kabla ya Julai 31, ambao ndiyo mwisho wa mkataba wake. Hatutatoa nyongeza nyingine kwa sababu tayari aliongezewa muda mwezi Machi," alisema.
Ndejembi alisema Kituo cha Hale kilipoanza kazi baada ya Uhuru kilikuwa kinazalisha megawati 21, kiwango ambacho wakati huo kilitosheleza mahitaji ya taifa yaliyokuwa takribani megawati 36. Hata hivyo, kutokana na uchakavu wa mitambo iliyodumu kwa zaidi ya miaka 60, uwezo wa uzalishaji uliporomoka hadi kufikia megawati sita pekee.
Alieleza kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kushirikiana na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden (SIDA), ilifadhili ukarabati wa kituo hicho kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 64, ambapo Tanzania imechangia asilimia 40 na Sweden kupitia SIDA asilimia 60.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, fedha hizo zimetumika kufunga mitambo mipya ya kisasa yenye uwezo wa kurejesha uzalishaji wa megawati 21 pamoja na kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa umeme.
Alisema hadi sasa asilimia 98 ya vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kukamilisha mradi vimewasili eneo la kazi na mafundi wanaendelea na hatua za mwisho za ufungaji, jambo linalotoa matumaini ya mradi kukamilika kwa wakati.
Ndejembi alisema mradi huo pia unahusisha ufungaji wa transfoma kubwa yenye uwezo wa kupokea na kusambaza umeme mwingi zaidi pamoja na uingizwaji wa nyaya za zamani zilizowekwa mwaka 1964 ambazo zilikuwa na uwezo mdogo wa kusafirisha umeme.
Alisisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha Gridi ya Taifa na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Kaskazini, hususan Mkoa wa Tanga ambao kwa sasa unatumia takribani megawati 130 kutokana na kukua kwa shughuli za viwanda na uchumi.
"Umeme si anasa, ni hitaji la msingi kwa maendeleo ya sekta za afya, elimu, viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji," alisema.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji Umeme wa TANESCO, Timothy Mgaya, alisema taasisi hiyo imepokea maelekezo ya serikali na itaendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha anakamilisha mradi kwa mujibu wa masharti ya mkataba.
Alisema endapo kutabainika ukiukwaji wowote wa masharti ya mkataba, hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria na makubaliano yaliyopo.
Mradi wa ukarabati wa Kituo cha Kufua Umeme cha Hale unagharimu dola za Marekani milioni 24.81, sawa na takribani shilingi bilioni 64. Hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 83, huku serikali ikisisitiza kuwa hakuna nyongeza nyingine ya muda itakayotolewa baada ya Julai 31 mwaka huu.






Post a Comment