WAZIRI NDEJEMBI ATOA MIEZI MIWILI KUKAMILISHA UMEME WA EACOP; MELI YA KWANZA YA MAFUTA KUTIA NANGA JANUARI 2027


WAZIRI NDEJEMBI ATOA MIEZI MIWILI KUKAMILISHA UMEME WA EACOP; MELI YA KWANZA YA MAFUTA KUTIA NANGA JANUARI 2027

Na Hadija Bagasha- Tanga

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amempa mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme chini ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) miezi miwili kuhakikisha anakamilisha njia maalumu ya kusafirisha umeme wa uhakika kwenda katika eneo la Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) lililopo Chongoleani, jijini Tanga.

Waziri huyo pia ametangaza kuwa meli ya kwanza ya kusafirisha mafuta ghafi kupitia Bandari ya Tanga inatarajiwa kutia nanga Januari 2027, huku mafuta yakitarajiwa kuanza kuwasili katika Kituo cha Chongoleani kuanzia Agosti mwaka huu, ishara kuwa mradi huo umeingia hatua za mwisho za utekelezaji.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo wa kimkakati, Ndejembi alisema Serikali haitavumilia ucheleweshaji wa utekelezaji wa miundombinu muhimu ya umeme inayohitajika kuhakikisha shughuli za EACOP zinaendelea bila changamoto za upatikanaji wa nishati.

Alisema, licha ya eneo la mradi tayari kuwa na huduma ya umeme, TANESCO inaendelea kujenga njia maalumu ya kusafirisha umeme kutoka Kituo Kikubwa cha Kupoza Umeme cha Majani Mapana ili kuhakikisha mradi unapata umeme wa uhakika wenye uwezo wa kukidhi mahitaji yote ya uendeshaji.

"Wakati wa kusuasua umekwisha. Mradi huu una ratiba maalumu ya utekelezaji na sekta ya nishati lazima iendane na kasi hiyo. Tunataka kuhakikisha miundombinu yote muhimu inakamilika kwa wakati," alisema Waziri Ndejembi.

Alieleza kuwa kukamilika kwa EACOP kutaifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda kwenda masoko ya kimataifa kupitia Bandari ya Tanga, hatua itakayoongeza nafasi ya nchi katika biashara ya kimataifa ya nishati pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Burian, alisema mradi huo umefikia takribani asilimia 90 ya utekelezaji na unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Tanga na Taifa kwa ujumla kupitia ajira, biashara, uwekezaji na ongezeko la mapato ya Serikali.

Naye Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Huduma wa Kampuni ya EACOP Tanzania, Geoffrey Mponda, alisema ujenzi wa mradi huo umefikia hatua za mwisho, huku maandalizi ya kukamilisha miundombinu yote muhimu yakiendelea ili kuhakikisha usafirishaji wa mafuta ghafi unaanza kwa wakati uliopangwa.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unahusisha ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga. Mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki na unatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania na Uganda kupitia sekta ya nishati, biashara na uwekezaji.



Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post