TAKUKURU TANGA YAOKOA ZAIDI YA SH. MILIONI 116 KUPITIA MFUMO WA NeST

TAKUKURU TANGA YAOKOA ZAIDI YA SH. MILIONI 116 KUPITIA MFUMO WA NeST

Na Hadija Bagasha, Tanga

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga imefanikiwa kuokoa zaidi ya Shilingi milioni 116.2 za Serikali zilizokuwa katika hatari ya kupotea baada ya kubaini na kurekebisha kasoro mbalimbali katika utekelezaji wa miradi ya elimu kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).


Mafanikio hayo yalielezwa na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Ramadhan Ndwata, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 8, 2026 kuhusu utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo katika robo ya kwanza ya mwaka kuanzia Januari hadi Machi 2026.


Ndwata alisema ufuatiliaji wa karibu wa TAKUKURU katika miradi ya maendeleo umebaini dosari kadhaa zilizokuwa zikikwamisha utekelezaji wa miradi ya elimu licha ya Serikali kuwa tayari imeshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.


Alitaja miongoni mwa miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa madarasa mawili pamoja na vyoo katika Shule ya Sekondari Chongoleani, ambao ulikwama tangu Machi 2024 kutokana na makadirio ya gharama za manunuzi kuwa chini ya bei halisi ya soko.



Kwa mujibu wa Ndwata, hali hiyo ilisababisha mfumo wa NeST kukataa zabuni zote zilizowasilishwa kwa kuwa hazikukidhi vigezo vya kitaalamu vinavyotakiwa.

Aidha, alisema mradi mwingine wa ujenzi wa vyoo wenye thamani ya Shilingi milioni 40 katika shule hiyo ulikumbwa na changamoto ya kutokuwa na makadirio ya gharama yaliyoandaliwa, jambo lililosababisha mchakato wa manunuzi kushindwa kuanza na hivyo kuchelewesha utekelezaji wake.


“Kwa upande wa ujenzi wa vyoo vya Shilingi milioni 40 katika Shule ya Sekondari Chongoleani, hakukuwa kabisa na makadirio ya gharama yaliyoandaliwa jambo lililosababisha mchakato kushindwa kuanza. Tulichukua hatua za dharura na kwa sasa mradi umerudi katika utekelezaji na unaendelea vizuri,” alisema Ndwata.


Katika hatua nyingine, TAKUKURU ilifuatilia mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kwabastola wilayani Muheza wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni moja, ambapo ilibaini baadhi ya kazi zilifanyika chini ya viwango vinavyotakiwa.


Kutokana na dosari hizo, taasisi hiyo ilielekeza marekebisho ya haraka ili kuhakikisha thamani ya fedha za Serikali inalindwa na wananchi wanapata huduma stahiki kutokana na uwekezaji huo mkubwa.


Baadhi ya kazi zilizorekebishwa ni pamoja na upakaji wa varnish kwenye milango, maboresho ya kazi za gypsum pamoja na kuhakikisha vifaa muhimu vya shule vinapatikana kwa wakati.


Ndwata alisema TAKUKURU pia ilisimamia ununuzi wa vitanda 57 vyenye thamani ya Shilingi milioni 22.4 kwa ajili ya shule hiyo, huku vitanda vingine 23 vilivyokuwa vimehamishiwa katika shule jirani vikielekezwa kurejeshwa ili vitumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa.


Mbali na usimamizi wa miradi ya maendeleo, TAKUKURU Mkoa wa Tanga imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kupitia utoaji wa elimu kwa umma.


Katika kipindi hicho, wananchi 189,521 walifikiwa kupitia semina, mikutano ya hadhara, vipindi vya uelimishaji na klabu za wapinga rushwa katika shule mbalimbali, hatua iliyolenga kuongeza uelewa kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa kulinda rasilimali za umma.


Kwa upande wa utekelezaji wa sheria, TAKUKURU ilipokea jumla ya malalamiko 133 katika robo ya kwanza ya mwaka, ambapo malalamiko 100 yalihusiana moja kwa moja na tuhuma za vitendo vya rushwa.


Ndwata alisema uchunguzi wa malalamiko hayo unaendelea kwa mujibu wa sheria, huku baadhi ya kesi tayari zikifikishwa mahakamani.


Alisema katika kipindi hicho jumla ya kesi 11 mpya zilifunguliwa mahakamani, wakati kesi nyingine 18 zikiendelea kusikilizwa katika mahakama mbalimbali mkoani Tanga.


Akizungumzia mipango ya robo ya pili ya mwaka kuanzia Aprili hadi Juni 2026, Ndwata alisema TAKUKURU itaendelea kufanya uchambuzi wa mifumo ya utendaji kazi katika taasisi za umma kwa lengo la kubaini na kuziba mianya ya rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya mali za umma.


Pia aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na ubadhirifu ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa na kutumika kwa manufaa ya wananchi wote.


“Mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushirikiano wa kila mwananchi. Tunapaswa kulinda rasilimali za taifa ili ziweze kuleta maendeleo na kuboresha maisha ya Watanzania wote,” alisisitiza Ndwata.


Hatua hizo zinaendelea kuonyesha umuhimu wa matumizi ya mifumo ya kidijitali kama NeST katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma, huku zikihakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post