RAIS WA CWT IKOMBA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA RUSHWA NA UHUJUMU UCHUMI
Na Arushadigital| Dodoma
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Suleiman Ikomba, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma leo Juni 8, 2026, na kusomewa mashtaka 14 yanayohusisha tuhuma za rushwa, kuunda genge la uhalifu na uhujumu uchumi.
Ikomba ni miongoni mwa viongozi wanane wa CWT wanaokabiliwa na mashtaka hayo yaliyofunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Washtakiwa wengine walifikishwa mahakamani Mei 25, 2026, huku Ikomba akiwa hakuwepo wakati huo.
Mbali na Ikomba, washtakiwa wengine katika shauri hilo ni aliyekuwa Rais wa CWT, Leah Ulaya, Maganga Japhet, Nashon Kidudu, Joseph Misalaba, Baraka Mbonalibha, Wambura Kihengu, Angelina Wambura pamoja na Kampuni ya Pyrite and Industries Company Limited.
Upande wa mashtaka unadai kuwa washtakiwa hao walijihusisha na vitendo vilivolisababishia CWT hasara kubwa ya kifedha, ikiwemo kujipatia zaidi ya Shilingi bilioni 2.2 kinyume na Katiba ya chama hicho.
Aidha, wanadaiwa kujinufaisha kwa zaidi ya Shilingi bilioni 1.3 kutoka Kampuni ya Pyrite and Industries Company Limited kwa lengo la kushawishi na kupitisha zabuni ya kutengeneza tisheti na kofia za CWT, kinyume na taratibu na sheria zilizopo.
Akizungumza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Denis Mpelembwa, Wakili wa Serikali, Gothard Mwingira, aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kwamba upande wa mashtaka unaendelea kukusanya ushahidi.
Kwa kuwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao ni ya uhujumu uchumi, Ikomba hakutakiwa kujibu chochote mahakamani katika hatua hiyo ya awali.
Mahakama imeutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi wa shauri hilo na kuwasilisha taarifa ya maendeleo ya kesi katika tarehe ijayo ya kutajwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 19, 2026, itakapotajwa tena mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
