MCHENGERWA: TAFITI ZIIMARISHWE KUKABILIANA NA MABADILIKO YA MALARIA
Na Joseph Ngilisho |ARUSHA
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amewataka watafiti nchini kuendelea kuimarisha tafiti za kisayansi zitakazosaidia kukabiliana na changamoto mpya zinazojitokeza katika mapambano dhidi ya malaria na magonjwa mengine ya kuambukiza, akisisitiza kuwa tafiti zina nafasi muhimu katika kuboresha afya za wananchi na maendeleo ya taifa.
Mchengerwa alitoa kauli hiyo jijini Arusha wakati akifungua Kongamano la 33 la Kisayansi la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa (NIMR), lililowakutanisha watafiti, wataalamu wa afya, wabunifu wa teknolojia za afya na wadau mbalimbali kujadili matokeo ya tafiti na mwelekeo wa sekta ya afya nchini.
Alisema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kupunguza maambukizi ya malaria nchini, ugonjwa huo bado unaendelea kuwa tishio la afya ya umma kutokana na mabadiliko ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa huo pamoja na usugu wa dawa na mbu wanaousambaza.
“Tunashuhudia mabadiliko mbalimbali katika magonjwa, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwekeza katika tafiti za kisayansi zitakazotupa majibu ya changamoto za sasa na zijazo. Tafiti ndiyo msingi wa maamuzi sahihi katika sekta ya afya,” alisema Mchengerwa.
Alibainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za utafiti, vyuo vikuu na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuzalisha maarifa na ubunifu unaoweza kusaidia kuboresha huduma za afya na kudhibiti magonjwa.
Waziri huyo aliwataka watafiti kuhakikisha matokeo ya tafiti wanazozifanya yanatumika katika kuandaa sera, mipango na mikakati ya afya yenye kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Alisema tafiti zinapaswa kuelekezwa katika kutatua changamoto halisi zinazowakabili wananchi na kusaidia Serikali kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi wa kisayansi.
Mchengerwa pia aliipongeza NIMR kwa mchango wake mkubwa katika kuzalisha tafiti zenye manufaa kwa taifa na kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na kimataifa katika nyanja za utafiti wa afya.
Kwa upande wake, uongozi wa NIMR ulieleza kuwa kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kuwasilisha matokeo ya tafiti mbalimbali na kujadili namna bora ya kuyatumia katika kuboresha huduma za afya nchini.
Kongamano hilo la 33 limewakutanisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, huku likijadili masuala mbalimbali ya afya ikiwemo malaria, magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza na matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma za afya.
Ends..
