WAZIRI WA AFYA MCHENGERWA: TAFITI ZIENDELEE KUTOA MAJIBU YA CHANGAMOTO ZA AFYA TANZANIA
Na Joseph Ngilisho|ARUSHA
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema tafiti za afya zimeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kusaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi na kuboresha huduma za afya kwa wananchi, huku akizitaka taasisi za utafiti nchini kuendelea kutafuta majawabu ya changamoto mpya na zinazoibuka katika sekta ya afya.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 33 la Kisayansi la Taasisi ya Taifa ya utafiti wa Magongwa (NIMR), Mchengerwa alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa tafiti za afya katika kuimarisha mifumo ya huduma za afya na kuboresha maisha ya Watanzania.
Alisema kupitia tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini, Tanzania imefanikiwa kupata ushahidi wa kisayansi uliosaidia katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, yakiwemo UKIMWI, malaria, kifua kikuu, saratani na kisukari.
“Matokeo ya tafiti hizi yamekuwa msingi muhimu wa kupanga sera, mikakati na afua mbalimbali za afya zinazolenga kuboresha huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa mfumo wa afya,” alisema Mchengerwa.
Waziri huyo aliipongeza NIMR kwa kuendelea kuongoza tafiti za afya nchini na kushirikiana na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi katika kutafuta suluhisho la changamoto za kiafya zinazowakabili Watanzania na dunia kwa ujumla.
Aidha, alisema matumizi ya teknolojia katika tafiti za afya yameongeza uwezo wa watafiti kukusanya na kuchambua taarifa kwa haraka zaidi, hali inayosaidia kupata matokeo yenye tija kwa maendeleo ya sekta ya afya.
Mchengerwa pia aliwahimiza watafiti kuendelea kufanya tafiti zinazolenga mahitaji halisi ya wananchi na kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika katika kuboresha huduma za afya, badala ya kubaki kwenye machapisho ya kitaaluma pekee.
Alibainisha kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za utafiti kwa kuimarisha mazingira ya kazi kwa watafiti na kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za utafiti, vyuo vikuu na wadau wa maendeleo.
Katika kongamano hilo la 33 la kisayansi, washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania walikutana kujadili matokeo ya tafiti mbalimbali za afya, kubadilishana uzoefu na kuibua mikakati ya kukabiliana na changamoto za afya zinazojitokeza nchini, barani Afrika na duniani.
***Ends***


