MOUNT MERU YAPUNGUZA VIFO VYA UZAZI KUTOKA 32 HADI 11, YAOMBA KUONGEZEWA WATAALAMU WA AFYA

MOUNT MERU YAPUNGUZA VIFO VYA UZAZI KUTOKA 32 HADI 11, YAOMBA KUONGEZEWA WATAALAMU WA AFYA

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA 

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mount Meru jijini Arusha imefanikiwa kupunguza vifo vya uzazi kutoka vifo 32 kwa mwaka hadi kufikia vifo 11 pekee, huku ikiiomba Serikali kuendelea kuimarisha upatikanaji wa wataalamu wa afya ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya huduma za matibabu.

Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Ernest Alex, wakati akitoa hotuba katika hafla ya uzinduzi wa Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mount Meru, uliofanywa na Waziri wa Afya, , jijini Arusha.

Dkt. Alex alisema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, , pamoja na juhudi za watumishi wa afya katika kuboresha huduma za uzazi na mtoto.

Alisema Hospitali ya Mount Meru, ambayo ilianzishwa zaidi ya miaka 100 iliyopita kwa ajili ya kuhudumia majeruhi wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, kwa sasa imekuwa nguzo muhimu ya utoaji wa huduma za afya katika Ukanda wa Kaskazini, ikihudumia wakazi zaidi ya milioni 2.3 wa Mkoa wa Arusha na wagonjwa wa rufaa kutoka mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Singida.

Kwa mujibu wa Dkt. Alex, hospitali hiyo yenye uwezo wa vitanda 450 hupokea kati ya wagonjwa 700 hadi 1,200 wa nje kila siku, huku idadi ya wagonjwa wanaolazwa kwa wakati mmoja ikifikia kati ya 200 na 300.

Alisema hospitali imeendelea kuimarisha huduma zake katika idara mbalimbali za tiba, upasuaji, magonjwa ya watoto, uzazi, mifupa, mfumo wa mkojo (urology), huduma za wagonjwa mahututi (ICU), huduma za watoto wachanga mahututi (Neonatal ICU) pamoja na uchunguzi na matibabu ya saratani.

“Kwa kufuata miongozo ya Wizara ya Afya kuhusu huduma salama za uzazi, tumefanikiwa kupunguza vifo vya uzazi kutoka 32 mwaka 2020/2021 hadi kufikia vifo 11 mwaka 2024/2025. Dhamira yetu ni kufikia sifuri ya vifo vya uzazi vinavyoweza kuzuilika,” alisema.

Aidha, alisema idadi ya wagonjwa wa nje imeongezeka kwa takribani asilimia 22 kutokana na kuimarika kwa huduma za maabara, vifaa vya uchunguzi wa kisasa na kuongezeka kwa imani ya wananchi kwa huduma zinazotolewa hospitalini hapo.

Katika upande wa mapato, Dkt. Alex alisema matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato na udhibiti wa mianya ya upotevu wa fedha yamewezesha mapato ya ndani kuongezeka kutoka Shilingi bilioni 2.8 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 11.9 mwaka wa fedha 2024/2025.

Alisema ongezeko hilo limeiwezesha hospitali kununua dawa za dharura, kuboresha miundombinu, kufanya matengenezo ya vifaa tiba na kuongeza motisha kwa watumishi.

Dkt. Alex alimshukuru Rais Samia kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika hospitalini hapo, ukiwemo ujenzi wa jengo la kisasa la huduma za dharura (Emergency Department), uboreshaji wa vitengo vya wagonjwa mahututi kwa watu wazima na watoto pamoja na Neonatal ICU.

Alisema uwekezaji huo umechangia kuokoa maisha ya maelfu ya watoto wachanga waliokuwa katika hatari kutokana na kuzaliwa kabla ya muda au matatizo ya upumuaji.

Kwa upande wa teknolojia, alisema hospitali imeimarisha huduma za uchunguzi kwa kuwa na mashine ya kisasa ya CT Scan yenye uwezo wa Slice 64, mashine za kisasa za X-Ray na Ultrasound pamoja na maabara iliyopata ithibati ya kimataifa ya ubora wa huduma.

Aidha, hospitali imekamilisha mradi wa uzalishaji wa oksijeni ambao kwa sasa unakidhi mahitaji yote ya hospitali na kuzalisha ziada inayosambazwa katika hospitali za wilaya za Mkoa wa Arusha.

Hata hivyo, Dkt. Alex alisema hospitali bado inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa wataalamu wa afya, ikifanya kazi na asilimia 48 pekee ya watumishi wanaohitajika kwa mujibu wa muundo wake.

Alitaja kada zenye upungufu mkubwa kuwa ni madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo, saratani, wagonjwa mahututi na upasuaji wa ubongo (neurosurgery), hali inayowalazimu watumishi waliopo kufanya kazi kwa muda mrefu na kusababisha uchovu wa kitaaluma.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutupatia watumishi zaidi ya 120 katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, lakini bado mahitaji ni makubwa kutokana na ongezeko la wagonjwa na huduma zinazotolewa hospitalini,” alisema.

Aliongeza kuwa uzinduzi wa bodi mpya ya hospitali hiyo unatoa fursa ya kuimarisha zaidi usimamizi wa taasisi, kuongeza uwajibikaji na kuharakisha utekelezaji wa mikakati ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Arusha na Ukanda mzima wa Kaskazini.

**Ends**

Post a Comment

Previous Post Next Post