KAMPENI YA UANDIKAJI WA WOSIA YASHIKA KASI NCHINI, WAJANE KUNUFAIKA NA ELIMU YA MIRATHI NA UTALII

 KAMPENI YA UANDIKAJI WA WOSIA YASHIKA KASI NCHINI, WAJANE KUNUFAIKA NA ELIMU YA MIRATHI NA UTALII

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Shirika la Kuendeleza na Kuwezesha Wajane Tanzania (Tanzania Widows Initiative Association - TAWIA) limezindua kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha wananchi kuandika wosia, hatua inayolenga kupunguza migogoro ya mirathi ambayo imekuwa chanzo cha mateso kwa wajane, watoto yatima na familia nyingi nchini.

Kampeni hiyo, inayofanyika chini ya mwamvuli wa Kilimanjaro Widows Summit, imeanza kupamba moto kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Juni 23. Mwaka huu Tanzania inaadhimisha miaka 12 tangu kuanza kwa maadhimisho hayo, huku wadau mbalimbali wakitumia fursa hiyo kuibua mijadala kuhusu haki za wajane na ustawi wa familia.

Akizungumza jijini Arusha, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa TAWIA, Rose William Sarwa, alisema taasisi hiyo imeamua kutumia maadhimisho ya mwaka huu kuhamasisha uandishi wa wosia kupitia kaulimbiu isemayo, “Andika Wosia Kuepuka Migogoro ya Mirathi Isiyo ya Lazima.”

Alisema lengo kuu la kampeni hiyo ni kujenga uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kupanga na kusimamia urithi kwa njia ya kisheria ili kuondoa migogoro inayojitokeza baada ya vifo vya wapendwa.

“Wosia si uchuro wala mwaliko wa kifo. Wosia ni ishara ya upendo, uwajibikaji na ulinzi kwa familia yako. Unasaidia kuelekeza namna mali na masuala mengine ya kifamilia yatakavyosimamiwa baada ya kifo cha mhusika, hivyo kuzuia migogoro na migawanyiko isiyo ya lazima,” alisema Sarwa.

Alifafanua kuwa TAWIA ilianzishwa mwaka 2014 na kwa sasa ina zaidi ya wanachama 700 nchini kote, huku ikiendelea kushirikiana na vikundi vya wajane, waratibu wa mikoa na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na utetezi wa haki za wajane.

Kwa mujibu wake, migogoro ya mirathi imeendelea kuwa changamoto kubwa inayowaathiri wajane wengi baada ya kupoteza wenza wao, hali inayosababisha baadhi yao kunyimwa haki za msingi za kumiliki mali za familia na kuingia katika migogoro mirefu ya kisheria.

Katika kuipa uzito kampeni hiyo, TAWIA ilianzisha safari maalumu ya kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia Juni 6 hadi 11 mwaka huu, ambapo ujumbe wa kuhamasisha uandishi wa wosia ulipelekwa hadi kileleni mwa mlima huo kama ishara ya kueneza mwamko mpya wa kulinda familia na haki za wajane.

“Tuliamini kuwa kufikisha ujumbe huu katika kilele cha Afrika ni hatua ya kuonyesha kuwa elimu ya mirathi na uandishi wa wosia inapaswa kuwafikia Watanzania wote bila kujali eneo walipo. Tunataka kuona nuru mpya ya matumaini ikiingia katika maisha ya wajane na familia nyingi nchini,” alisema.

Wakati kampeni hiyo ikiendelea kushika kasi, sekta ya utalii nayo imejitokeza kuunga mkono juhudi hizo kwa vitendo kupitia programu maalumu za kuwawezesha wajane kutembelea vivutio vya utalii.

Mkurugenzi wa Beric Tanzania Tours, Betty Gilbert, alisema kampuni yake kwa kushirikiana na washirika kutoka Kenya imefadhili safari za utalii kwa wajane wanaoshiriki kampeni hiyo ili kuwapa nafasi ya kupata uzoefu mpya, kujifunza na kujenga upya matumaini ya maisha.

Alisema wajane hao watatembelea Hifadhi za Taifa za Tarangire, Serengeti, Ziwa Manyara pamoja na Eneo la Hifadhi la Ngorongoro, maeneo yanayotambulika kimataifa kwa utajiri wake wa maliasili na vivutio vya utalii.

“Kama kampuni tunaamini kuwahudumia wenye mahitaji maalumu ni sehemu ya wajibu wetu kwa jamii. Uwezo tulionao ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo tunapaswa kuutumia kuwainua na kuwafariji wengine, hususan wajane wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha,” alisema Gilbert.

Aliongeza kuwa ushiriki wake katika kampeni hiyo umetokana na kuguswa binafsi na changamoto zinazowakabili wajane wengi nchini, akieleza kuwa safari hizo zitakuwa sehemu ya kuwapa faraja na motisha ya kuendelea kupambana na changamoto za maisha.

“Ninaamini tabasamu na furaha watakazopata wajane hawa vitakuwa zawadi kubwa kwetu. Tunatarajia safari hizi zitawajengea matumaini mapya na kuwapa nafasi ya kuona fursa zilizopo katika sekta ya utalii,” alisema.

Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranqhe, amepongeza juhudi zinazofanywa na TAWIA na kutangaza kuwa atakuwa mmoja wa mabalozi wa kampeni hiyo ya kitaifa.

Iranqhe alisema uandishi wa wosia ni nyenzo muhimu katika kulinda amani ya familia na kupunguza migogoro ya mirathi ambayo imekuwa ikisababisha migawanyiko, uhasama na kesi zisizoisha katika familia nyingi.

“Hii ni kampeni yenye manufaa makubwa kwa taifa. Nitaendelea kuwa balozi wa kuhamasisha wananchi kuelewa umuhimu wa kuandika wosia ili kulinda haki za wajane, watoto na kuimarisha mshikamano wa familia,” alisema.

Alisema uzoefu wake katika uongozi umemwezesha kushuhudia changamoto nyingi wanazokutana nazo wajane baada ya vifo vya wenza wao, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuimarisha elimu ya mirathi na mipango ya urithi.

Meya huyo pia alibainisha kuwa anatarajia kuandika kuhusu masuala ya wajane katika moja ya sura za kitabu anachoandaa, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu changamoto wanazopitia wajane na njia za kuzitatua.

Kampeni ya Kilimanjaro Widows Summit inatarajiwa kuendelea katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuhamasisha uandishi wa wosia kama sehemu ya kujenga familia zenye amani, kulinda haki za wajane na watoto, pamoja na kuondoa migogoro ya mirathi ambayo imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Post a Comment

أحدث أقدم