WARAKA WA TATU WA SABINA JOHN MOSI: MKAZO UNAOTOKANA NA DHULUMA YA MALI NA TUMAINI LA KUPATA HAKI

 

WARAKA WA TATU WA SABINA JOHN MOSI: MKAZO UNAOTOKANA NA DHULUMA YA MALI NA TUMAINI LA KUPATA HAKI

Na Sabina John Mosi

Huu ni waraka wangu wa tatu kuzungumzia mkazo wa maisha unaotokana na kile ninachokieleza kuwa ni dhuluma ya mali, changamoto ambayo kwa miaka kadhaa imeathiri maisha yangu, familia yangu na utekelezaji wa ndoto zangu za kuwahudumia watu kupitia miradi mbalimbali ya kijamii.


Natanguliza shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima, afya, akili, hekima, nguvu na uwezo wa kuendelea kusimama licha ya mawimbi makubwa ya changamoto nilizokutana nazo. Pia nawashukuru wanafamilia, marafiki na wananchi mbalimbali ambao wameendelea kunitia moyo katika kipindi hiki kigumu.


Nimeamua kuandika waraka huu kwa sababu naamini kuwa kuna maelfu ya Watanzania wanaopitia hali kama ninayopitia mimi. Wapo waliopoteza mali, haki zao au fursa zao kutokana na migogoro mbalimbali, na wengi wao wamebaki na majeraha ya kimwili, kiakili na kiuchumi.


Kabla ya changamoto hizi, nilikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na mafanikio ya kiuchumi na uwezo wa kusaidia wengine. Nilijishughulisha na shughuli mbalimbali zilizonipa uwezo wa kuhudumia familia, marafiki na watu wenye uhitaji.


 Hata hivyo, migogoro ya kifamilia na changamoto nyingine zilizosababisha mali zangu kuingia katika mkwamo wa muda mrefu zilinifanya nipoteze sehemu kubwa ya utajiri wangu na kuingia katika kipindi kigumu cha maisha.


Kutoka katika hali ya kuwa mtoaji wa msaada hadi kuwa mtu anayehitaji msaada na haki imekuwa safari yenye mafunzo makubwa. Nimejifunza kuwa mali inaweza kupotea, lakini utu, imani na matumaini havipaswi kupotea.


Mkazo unaotokana na dhuluma ya mali si jambo dogo. Athari zake huenea kwa familia nzima. Wazazi hukosa msaada walioutegemea, watoto hupata ugumu wa kupata elimu na mahitaji muhimu, huku vijana wanaotegemewa kuwa viongozi wa kesho wakikabiliwa na hali ya kukata tamaa. Hali hii imegusa hata watu waliokuwa wakitegemea huduma na msaada kupitia miradi yangu ya Nuru na Melita Hope.


Pamoja na hayo, ninaendelea kuamini kuwa Tanzania ni nchi inayojengwa juu ya misingi ya haki, usawa na utawala wa sheria. Ninaamini kuwa hakuna mwananchi anayepaswa kunyimwa haki kwa sababu ya kutokuwa kiongozi, tajiri au mwenye ushawishi mkubwa.


 Haki ni haki kwa kila mtu.

Ndiyo maana ninaendelea kuwa na matumaini kwamba siku moja nitapata stahiki zangu kwa mujibu wa sheria na kwamba mali na rasilimali zilizokwama kwa muda mrefu zitapatikana ili ziweze kusaidia familia yangu na jamii inayotegemea mchango wangu.


Kupitia waraka huu wa tatu, ninapenda kuwahimiza vijana kutokata tamaa wanapokutana na changamoto za maisha. Wajue kuwa wao ni wafalme na si watumwa wa mazingira wanayokutana nayo leo. 


Waweke akili zao katika maarifa, kazi, maadili mema na kumtegemea Mungu.


Ninawasihi pia kuthamini elimu kwa kuwa maarifa ndiyo ufunguo wa ukombozi wa kweli. Taifa au mtu anayepuuza maarifa hujiweka katika hatari ya kupoteza mwelekeo wa maisha na maendeleo yake.


Katika kipindi hiki kigumu, nimeendelea kushikilia imani kwamba Mungu ndiye hakimu wa mwisho wa kila jambo. Maandiko matakatifu yanatukumbusha kwamba mapito hupita na kwamba anayevumilia hadi mwisho ndiye mshindi.


Waraka huu wa tatu si kilio cha kukata tamaa, bali ni sauti ya matumaini. Ni ujumbe wa kuhimiza jamii kutambua madhara ya dhuluma, kuthamini haki na kuendelea kusimama imara hata wakati wa majaribu makubwa.


Ninaamini kuwa kwa imani, uvumilivu, maarifa na msaada wa Mungu, kila mkazo una mwisho wake. Naamini kuwa siku za mbele zinaweza kuwa bora kuliko za jana, na kwamba haki ikisimama, maisha ya wengi yanaweza kubadilika kuwa bora zaidi.

Itaendelea.....

Post a Comment

أحدث أقدم