HALMASHAURI YA LONGIDO YAPATA HATI SAFI MIAKA MITATU MFULULIZO, YAAHIDI KUFUNGA HOJA ZILIZOSALIA
Na Joseph Ngilisho| LONGIDO
HALMASHAURI ya Wilaya ya Longido imeendelea kudhihirisha usimamizi mzuri wa fedha za umma baada ya kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ikiwa ni mwaka wa tatu mfululizo kupata mafanikio hayo katika ukaguzi unaofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mafanikio hayo yalibainishwa katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani uliofanyika Juni 26, 2026, ambapo wajumbe walijadili taarifa ya hoja za ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na hatua zilizochukuliwa katika kuzitekeleza.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa Halmashauri ya Longido, Mboje Makeleja, alisema halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 42 za ukaguzi, zikiwemo hoja saba za miaka iliyopita na hoja 35 za mwaka wa fedha 2024/2025.
Alieleza kuwa kati ya hoja saba za nyuma, hoja tatu zimefungwa na kubaki nne, huku kati ya hoja 35 za mwaka 2024/2025, hoja 19 zikiwa zimetekelezwa na kufungwa, na hoja 16 zilizobaki zikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Makeleja alisema kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo ni ishara ya kuimarika kwa mifumo ya usimamizi wa fedha na uwajibikaji ndani ya halmashauri hiyo, akitoa pongezi kwa Mwenyekiti wa Halmashauri, Baraza la Madiwani, Mkurugenzi, timu ya menejimenti na watumishi wote kwa mchango wao katika mafanikio hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amezipongeza halmashauri zote saba za mkoa huo kwa kupata hati safi, akisema hatua hiyo inaongeza imani ya wananchi katika matumizi ya fedha za umma na kuonyesha kuimarika kwa uwajibikaji wa taasisi za serikali za mitaa.
Hata hivyo, aliwataka viongozi wa halmashauri kuhakikisha hoja zote ambazo bado zipo kwenye hatua za utekelezaji zinamaliziwa kwa wakati ili zifungwe kabisa, huku wakidumisha mifumo madhubuti ya kudhibiti mapato na matumizi ya fedha za serikali.
"Kupata hati safi ni jambo zuri, lakini ni muhimu kuhakikisha kunakuwa na udhibiti madhubuti wa mapato. Unaweza kuwa na hati safi, lakini kama hakuna usimamizi mzuri wa mapato na matumizi yake kwa kuzingatia taratibu za fedha, mafanikio hayo hayatakuwa na tija inayokusudiwa," alisema Makalla.
Aliongeza kuwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinapaswa kutumika kwa ufanisi ili miradi hiyo ikamilike kwa viwango vinavyostahili na kuendana na thamani halisi ya fedha za umma.
Ends..












إرسال تعليق