WANANCHI 67 WALALA NJE BAADA YA NYUMBA KUBOMOLEWA MUHEZA, WAMWOMBA RAIS SAMIA KUINGILIA KATI
Na Hadija Bagasha, Tanga
Simanzi, vilio na hali ya kukata tamaa vimetanda katika Kitongoji cha Bago, Kata ya Kigombe wilayani Muheza mkoani Tanga, baada ya wananchi wa kaya 67 kubaki bila makazi kufuatia kubomolewa kwa nyumba zao katika operesheni iliyotekelezwa Mei 22, mwaka huu.
Wananchi hao, wengi wao wakiwa familia za wafanyakazi wa zamani na vibarua wa mashamba ya mkonge, sasa wanaishi chini ya miti huku wakikabiliwa na ukosefu wa makazi, chakula, usalama na huduma nyingine muhimu za kijamii. Kutokana na hali hiyo, wamemuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati ili kupatikana suluhisho la haraka la mgogoro huo.
Uharibifu huo ulitokea katika Kijiji cha Msakangoto ambapo Kampuni ya Amboni Plantation, inayojihusisha na kilimo cha mkonge, ilitekeleza amri ya mahakama ya kuwaondoa wakazi hao katika eneo linalodaiwa kuwa mali ya kampuni hiyo.
Hata hivyo, waathirika wa tukio hilo wanadai kuwa utekelezaji wa amri hiyo ulifanyika katika mazingira yenye sintofahamu, huku baadhi yao wakieleza kuwa walikuta nyumba zao tayari zimebomolewa waliporejea kutoka kwenye shughuli za mashambani.
Mbali na kupoteza makazi, wananchi hao wanasema walipoteza mali zao mbalimbali zikiwemo fedha taslimu, mazao ya chakula, samani za nyumbani, vyombo na vifaa vya shule vya watoto, jambo ambalo limezidisha mateso kwa familia nyingi zilizokuwa tayari zikikabiliwa na hali ngumu ya maisha.
Akizungumza kwa uchungu, mmoja wa waathirika hao, Jane Sekela, alisema tukio hilo limewaacha wakiwa hawana matumaini ya maisha na kujihisi kama wakimbizi ndani ya nchi yao wenyewe.
“Sisi ni Watanzania lakini leo tunaishi kama wakimbizi. Mimi ni mama mwenye watoto wanane, sina mahali pa kuishi na mpaka sasa nalala nje. Tumepoteza kila kitu tulichokuwa nacho. Tunamuomba Rais Samia asikie kilio chetu na atusaidie kwa sababu tumedhalilishwa na kunyanyaswa,” alisema.
Kwa upande wake, Eva Stephen alisema watoto wameathirika zaidi kutokana na tukio hilo, hasa wanaojiandaa kufanya mitihani ya kitaifa.
Alisema aliporejea kutoka shambani alikuta nyumba yake ikiwa tayari imebomolewa na juhudi zake za kuokoa mali zilikuwa ndogo kutokana na kasi ya operesheni hiyo.
“Nilifanikiwa kuokoa baadhi ya vifaa vya shule vya watoto wangu, lakini vitu vingine vyote vilipotea. Watoto wameathirika kisaikolojia na hali hii imewavuruga sana wakati huu muhimu wa masomo yao,” alisema.
Naye Jane Francis alisema hali ya maisha kwa sasa ni ngumu kutokana na familia nyingi kulazimika kuishi nje bila makazi ya kudumu.
“Tunalala chini ya miti pamoja na watoto wetu. Madaftari, vitabu na vifaa vingine vya shule vimeharibika au kufukiwa kwenye vifusi. Hatujui kesho yetu itakuwaje. Tunaiomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma,” alisema.
Mmoja wa wakazi hao, Ally Mohamed, alisema tukio hilo limewaacha wananchi wengi na maswali kuhusu namna operesheni hiyo ilivyotekelezwa.
“Tulikuwa tunaona matukio kama haya yakitokea sehemu nyingine kupitia televisheni, lakini leo yametokea hapa kwetu. Hii ni hali inayoumiza na kuibua maswali mengi kuhusu haki za wananchi,” alisema.
Kutokana na malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, ameunda kamati maalumu kuchunguza mazingira yote yaliyozunguka utekelezaji wa amri hiyo ya mahakama.
Dkt. Burian alisema licha ya kuwepo kwa amri ya mahakama, bado kuna masuala muhimu yanayohitaji kufanyiwa tathmini ili kubaini kama taratibu zote zilifuatwa na haki za wananchi zilizingatiwa wakati wa utekelezaji wake.
Alisema kamati hiyo itachunguza kwa kina mchakato mzima wa operesheni hiyo, ikiwemo sababu za kutoshirikishwa kwa baadhi ya mamlaka husika pamoja na kujiridhisha kama maandalizi ya kuwapatia wananchi makazi mbadala na huduma muhimu yalifanyika kabla ya kuanza kwa zoezi hilo.
“Ni kweli kulikuwa na utekelezaji wa amri ya mahakama, lakini kuna masuala mbalimbali yanayohitaji kufanyiwa tathmini. Tumeunda timu maalumu ili kufuatilia na kujiridhisha kuhusu hatua zote zilizochukuliwa katika mchakato huo,” alisema Dkt. Burian.
Aliongeza kuwa kamati hiyo itatoa mapendekezo yatakayosaidia kubaini ukweli wa tukio hilo na kuhakikisha haki inapatikana kwa pande zote zinazohusika.
Wakati uchunguzi huo ukiendelea, waathirika wa tukio hilo wanaendelea kuishi katika mazingira magumu wakisubiri hatua za Serikali, huku wakitumaini kuwa kilio chao kitasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi utakaorejesha matumaini ya maisha yao baada ya kupoteza makazi na mali walizokuwa wamejenga kwa miaka mingi.






إرسال تعليق