DC KARATU AONGOZA UTATUZI WA MIGOGORO MARELA, ATOA MAAGIZO KUHUSU MAPATO YA KIJIJI
Na Joseph Ngilisho | KARATU
Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dkt. Lameck Karanga, ameongoza utatuzi wa migogoro na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa Kijiji cha Marera katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika kudumisha amani na kuharakisha maendeleo.
Katika mkutano huo uliowakutanisha viongozi wa vijiji na vitongoji, watendaji wa kata pamoja na wananchi, Dkt. Karanga alipokea na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa eneo hilo na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuzitafutia ufumbuzi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Alisema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itaendelea kuwa karibu na wananchi kwa lengo la kusikiliza na kutatua migogoro inayoweza kuathiri ustawi wa jamii na maendeleo ya kijiji.
“Ushirikiano kati ya wananchi na viongozi ni msingi muhimu wa kudumisha amani, mshikamano na maendeleo. Serikali itaendelea kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa haki,” alisema Dkt. Karanga.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka viongozi wa Kijiji cha Marera na vitongoji vyake kusimamia kwa umakini matumizi ya mapato ya asilimia 10 ya kijiji ili fedha hizo zielekezwe katika miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi.
Alieleza kuwa mapato hayo yanapaswa kutumika katika sekta muhimu za kijamii kama elimu, afya, maji na uboreshaji wa miundombinu, ili kuongeza kasi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.
Pia alisisitiza uwajibikaji, uwazi na matumizi sahihi ya fedha za umma, akionya dhidi ya vitendo vya ubadhirifu na matumizi yasiyo na tija ambayo yanaweza kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Serikali itaendelea kufuatilia matumizi ya mapato ya vijiji ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi,” alisisitiza.
Kwa upande wao, wananchi wa Marera walitumia mkutano huo kueleza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili, huku baadhi yao wakimpongeza Dkt. Karanga kwa kufika kijijini hapo na kusikiliza matatizo yao moja kwa moja.
Mkutano huo umeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali ya Wilaya ya Karatu za kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi na utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika ngazi ya kijiji.

إرسال تعليق