EALA YAUNGA MKONO BAJETI YA NYONGEZA YA DOLA MILIONI 4.7, YAANDAA KUPITISHA BAJETI YA MWAKA 2026/2027
Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
Kamati ya Bajeti ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) imewasilisha bungeni taarifa inayohusu ombi la bajeti ya nyongeza ya dola za Marekani milioni 4.7 lililowasilishwa na Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), huku ikipendekeza bunge liridhie matumizi hayo kwa kuwa ni halali na muhimu kwa utekelezaji wa miradi na programu za jumuiya hiyo.
Akizungumza baada ya kuwasilisha taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya EALA, Dkt Abdullah Makame , alisema fedha hizo tayari zimetumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofadhiliwa na wadau wa maendeleo, na kwamba kuchelewa kuwasilishwa kwa maombi hayo kulitokana na kutokuwepo kwa vikao vya Bunge la Afrika Mashariki na Baraza la Mawaziri kwa zaidi ya miezi sita.
Alieleza kuwa baada ya Baraza la Mawaziri kukutana na kupitia taarifa za mapato, matumizi na makadirio ya bajeti, liliridhika na maombi hayo na kuyawasilisha kwa Kamati ya Bajeti ya EALA kwa uchambuzi zaidi.
“Kamati iliyapitia na kuyajadili kwa kina, na hatimaye ikaamua kuwasilisha taarifa bungeni ili wabunge waridhie ombi la waziri wa Uganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC na Naibu Waziri Mkuu wa Uganda,” alisema.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, matumizi hayo yanahusiana na utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za maendeleo za EAC na yana manufaa kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Aidha, alisema kamati hiyo imekamilisha uchambuzi wa hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 iliyowasilishwa na waziri husika, na imefanya mashauriano ya karibu na uongozi wa sekretarieti pamoja na Baraza la Mawaziri.
Mwikya alisema kamati inatarajia kuwasilisha rasmi taarifa yake ya bajeti bungeni na kuomba wabunge kuipitisha, huku ikiwasilisha marekebisho madogo yaliyokubaliwa baada ya majadiliano na upande wa serikali.
Alibainisha kuwa makadirio ya awali ya bajeti yaliyowasilishwa na waziri yalikuwa dola za Marekani milioni 110, lakini baada ya marekebisho yaliyofanywa kwa mashauriano kati ya kamati na serikali, bajeti hiyo inatarajiwa kufikia dola milioni 112.
“Tunatarajia kupata uungwaji mkono wa wabunge na hatimaye kupitisha bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli na programu zilizopangwa,” alisema.
Kamati hiyo imeeleza matumaini kuwa kupitishwa kwa bajeti hiyo kutachochea utekelezaji wa miradi ya kikanda na kuimarisha ajenda ya ushirikiano na maendeleo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

إرسال تعليق