DREAMERS ACADEMY YAHAMASISHA WATOTO KUJIFUNZA KARATE
Na Joseph Ngilisho| ARUSHA
Mkurugenzi wa Dreamers Academy, Alex Felix, amewahimiza wazazi kuwapeleka watoto wao katika mafunzo ya karate akisema mchezo huo ni nyenzo muhimu ya kuwajengea watoto nidhamu, kujiamini na maadili bora yatakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.
Akizungumza wakati wa kutambulisha rasmi programu ya mafunzo ya karate kwa watoto jijini Arusha, Felix alisema Dreamers Academy imeanzishwa kwa lengo la kukuza vipaji vya watoto katika michezo mbalimbali ikiwemo karate, ndondi, kuogelea na michezo mingine, huku wakianza na karate kama hatua ya kwanza ya kutimiza ndoto hiyo.
Alisema mafunzo hayo yanawalenga watoto kuanzia umri wa miaka minne, akieleza kuwa umri huo ni muhimu katika kujenga msingi imara wa nidhamu na maendeleo ya mtoto kupitia michezo.
“Watu wengi wana mtazamo usio sahihi kuhusu karate. Karate si mchezo wa ugomvi wala vurugu. Ni mchezo unaofundisha heshima, uvumilivu, nidhamu, kujitambua na kujiamini. Tunawaomba wazazi wawaletee watoto wao ili waweze kujifunza maadili mazuri yatakayowasaidia katika maisha yao yote,” alisema Felix.
Alibainisha kuwa moja ya changamoto zinazokabili maendeleo ya karate mkoani Arusha ni idadi ndogo ya watoto wanaojitokeza kushiriki mchezo huo, hali inayochangiwa na uelewa mdogo wa baadhi ya wazazi kuhusu faida za karate.
Kwa mujibu wa Felix, kwa sasa Dreamers Academy inaendesha mafunzo katika vituo viwili vya Brotherhood Gym na Sinon, ambapo zaidi ya watoto 35 tayari wameanza kushiriki mazoezi hayo.
Alisema lengo lao ni kuona watoto wengi zaidi wakijiunga ili kuandaa kizazi kitakachoweza kushiriki mashindano ya mkoa, taifa na hata kimataifa katika siku zijazo.
“Karate ni msingi wa mafanikio katika michezo na maisha kwa ujumla. Ukiangalia mataifa yaliyoendelea katika michezo kama China na Japan, utaona wamewekeza sana katika kuwafundisha watoto nidhamu tangu wakiwa wadogo. Hilo ndilo tunalolenga kulifanya hapa Tanzania,” alisema.
Aidha, ameiomba Serikali kupitia shule za msingi kuangalia uwezekano wa kuingiza mafunzo ya karate katika shughuli za michezo mashuleni ili kuwasaidia watoto wengi zaidi kupata fursa ya kujifunza mchezo huo.
“Tunaiomba Serikali kushirikiana na wadau wa karate ili mchezo huu ufike kwa watoto wengi zaidi. Karate husaidia kujenga nidhamu, kujiamini na kuwalea watoto kuwa raia wema wa kesho,” alisema.
Felix aliongeza kuwa safari ya karate huanza kwa mkanda mweupe na kuendelea hatua kwa hatua hadi mkanda mweusi na madaraja mengine ya juu, huku akisisitiza kuwa karate ni elimu ya maisha inayohitaji kujifunza na kujiendeleza kila wakati.
Kwa sasa mafunzo ya karate katika Brotherhood Gym yanafanyika kila Jumamosi kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana, huku ratiba maalumu ya likizo ikiwezesha watoto kufanya mazoezi kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi.
Ends..





إرسال تعليق