Wanachama wa CCM Osunyai Waibua Kero za Uhalifu, Uchafu na Mradi wa Shule Kutelekezwa
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Osunyai, Jijini Arusha, wameibua kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa eneo hilo, zikiwemo ongezeko la uhalifu wa vibaka wanaowavamia wananchi usiku kwa visu na kuwapora mali zao, hali ya uchafu katika mitaa mbalimbali, wizi wa mita za maji pamoja na kusimama kwa mradi wa ujenzi wa ghorofa katika Shule ya Msingi Osunyai.
Kero hizo ziliibuliwa wakati wa mkutano wa ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM uliofanyika katika kata hiyo na kuhudhuriwa na viongozi wa chama, serikali za mitaa na wananchi.
Wanachama hao walieleza kuwa matukio ya uhalifu yameongezeka katika baadhi ya maeneo ya kata hiyo, huku vibaka wakidaiwa kuwashambulia wananchi nyakati za usiku kwa kutumia visu kabla ya kuwapora fedha na mali mbalimbali.
Mbali na changamoto hiyo, wananchi walilalamikia hali ya uchafu katika baadhi ya maeneo ya makazi, wakidai kuwa mazingira hayo yanahatarisha afya za wakazi na yanahitaji hatua za haraka za usafi na usimamizi wa taka.
Pia wananchi walieleza wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa matukio ya wizi wa mita za maji, hali inayosababisha hasara kwa wananchi pamoja na usumbufu wa huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.
Katika mkutano huo, baadhi ya wenyeviti wa mitaa walilalamikia hatua ya kupokonywa mihuri ya ofisi zao wakidai kuwa hali hiyo imekuwa ikitokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo ukosefu wa vitendea kazi na ushirikiano wa kutosha katika kutatua kero za wananchi.
Aidha, wananchi waliibua kwa uzito mkubwa suala la kusimama kwa mradi wa ujenzi wa jengo la ghorofa katika Shule ya Msingi Osunyai, ambapo eneo la mradi limegeuka bwawa la maji machafu yenye harufu kali baada ya mkandarasi kufanya uchimbaji na kisha kuondoka kwa madai ya kutolipwa fedha.
Wananchi walisema maji hayo yameendelea kuzingira sehemu ya shule na kuhatarisha afya za wanafunzi zaidi ya 3,000 wanaosoma katika shule hiyo, huku wakihofia uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko pamoja na ajali kwa watoto.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Arusha, Ally Mwinyimvua maarufu kwa jina la Meku, aliiomba Halmashauri ya Jiji la Arusha kuharakisha upatikanaji wa fedha kwa mkandarasi ili arejee eneo la mradi na kuukamilisha kwa wakati.
Alisema kuchelewa kwa mradi huo kumesababisha wanafunzi wengi kusoma katika mazingira ya msongamano mkubwa baada ya baadhi ya madarasa kubomolewa kupisha ujenzi wa ghorofa hilo.
“Tunaiomba Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhakikisha fedha zinapatikana haraka ili mradi huu ukamilike. Mbali na msongamano wa wanafunzi, eneo la mradi limejaa maji machafu ambayo ni hatari kwa afya na usalama wa watoto wetu,” alisema Mwinyimvua.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Osunyai, Elirehema Nnko, alisema mradi huo ulitengewa zaidi ya shilingi milioni 360 katika mwaka wa fedha 2024/2025, lakini ulisimama baada ya kubainika kuwepo kwa hitilafu katika ramani za awali za ujenzi.
Alisema tayari taratibu za kumpata mkandarasi mwingine zimekamilika na hatua zinazofuata ni kuhakikisha fedha zinapatikana ili ujenzi uanze tena na kukamilika kwa manufaa ya wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Wananchi wa Osunyai wamezitaka mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kutatua kero hizo ili kurejesha usalama, usafi wa mazingira na kuboresha huduma za kijamii katika kata hiyo.








إرسال تعليق