DKT. MUGOBI: KARIBU KILIFAIR INAENDELEA KUIFUNGULIA TANZANIA FURSA ZA UTALII NA UWEKEZAJI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA 

SERIKALI imesema Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu Kilifair yanaendelea kuwa moja ya majukwaa muhimu zaidi ya kuitangaza Tanzania katika soko la kimataifa, huku yakifungua milango ya uwekezaji, biashara na ushirikiano unaochochea ukuaji wa sekta ya utalii na uchumi wa taifa kwa ujumla.


Akifungua rasmi maonesho hayo jijini Arusha kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Utalii nchini, Dkt. Thereza Mugobi, alisema mafanikio makubwa ya Karibu Kilifair yanaakisi imani kubwa ambayo jumuiya ya kimataifa inaendelea kuwa nayo kwa Tanzania kama moja ya destinasheni bora za utalii na uwekezaji duniani.



Alisema toleo la mwaka huu limewakutanisha zaidi ya waoneshaji 1,560 pamoja na wanunuzi wa huduma za utalii zaidi ya 500 kutoka mataifa zaidi ya 40 duniani, hali inayodhihirisha kuongezeka kwa ushawishi wa Tanzania katika soko la kimataifa la utalii.


“Ushiriki huu mkubwa unaonesha wazi kuwa Tanzania inaendelea kuvutia wadau wa utalii kutoka pembe mbalimbali za dunia. Karibu Kilifair imekuwa daraja muhimu la kuunganisha biashara, uwekezaji na masoko mapya ya utalii,” alisema Dkt. Mugobi.


Alibainisha kuwa sekta ya utalii inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania kwa kuchangia asilimia 17.2 ya Pato la Taifa na kutoa zaidi ya ajira milioni 2.5 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa Watanzania.


Dkt. Mugobi alisema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya utalii, kuboresha huduma, kufungua masoko mapya na kuimarisha kampeni za kimataifa za kuitangaza Tanzania.


Kwa mujibu wake, hatua hizo zimechangia ongezeko kubwa la mapato ya utalii yaliyoongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi zaidi ya dola bilioni 4.4 kwa sasa, sambamba na kuongezeka kwa idadi ya watalii wa kimataifa wanaoitembelea Tanzania.


Akizungumzia juhudi za kuitangaza Tanzania duniani, Dkt. Mugobi alieleza kuwa uzinduzi wa filamu ya Tanzania: The African Dream ni sehemu ya mkakati wa kisasa wa kutumia simulizi za utalii kufikia masoko mapya na kuvutia wageni wengi zaidi.


Alisema filamu hiyo imeonesha kwa undani hazina ya vivutio vya Tanzania ikiwemo wanyamapori, mandhari za asili, urithi wa kihistoria, tamaduni mbalimbali, fukwe za Bahari ya Hindi pamoja na ukarimu wa wananchi wake.


“Tunatarajia filamu hii kuwa chombo muhimu cha kuitangaza Tanzania kwa mamilioni ya watazamaji duniani na kuwahamasisha kuichagua Tanzania kama sehemu yao ya safari na mapumziko,” alisema.


Dkt. Mugobi alitaja vivutio vikuu vinavyoendelea kuipa Tanzania umaarufu duniani kuwa ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Eneo la Hifadhi la Ngorongoro, fukwe za Zanzibar, vivutio vya ukanda wa kusini pamoja na maeneo mbalimbali ya urithi wa utamaduni.


Alisisitiza kuwa Karibu Kilifair si maonesho ya kawaida, bali ni uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuimarisha mustakabali wa utalii wa Tanzania kupitia kujenga mahusiano ya kibiashara, kuongeza idadi ya watalii, kuvutia wawekezaji wapya na kuimarisha uchumi wa wananchi wanaotegemea sekta hiyo.


Aidha, alisema Tanzania inaendelea kujipanga kutumia fursa ya kuandaa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 kwa ushirikiano na Kenya na Uganda kama jukwaa la kuitangaza nchi kupitia utalii, utamaduni, michezo na uwekezaji.


Alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya utalii, kuongeza ubora wa huduma za malazi, kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali na kuendeleza kampeni za masoko ili kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na tukio hilo la kihistoria.


Katika hitimisho la hotuba yake, Dkt. Mugobi aliwashukuru wadhamini, washirika wa maendeleo, waoneshaji na wanunuzi wa huduma za utalii kwa mchango wao katika kufanikisha maonesho hayo, huku akiwahimiza kutumia fursa hiyo kujenga ushirikiano mpya, kuendeleza biashara na kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa.


“Karibu Kilifair ni zaidi ya maonesho; ni jukwaa linaloendelea kuifungulia Tanzania milango ya maend

eleo ya kiuchumi kupitia sekta ya utalii,” alisema.






Ends..


Post a Comment

أحدث أقدم