Ukosefu wa Chakula Shuleni Waathiri Elimu Longido, CORDS Yaingilia Kati kwa Mradi Maalum
Na Joseph Ngilisho | LONGIDO
CHANGAMOTO ya ukosefu wa chakula mashuleni imeendelea kuathiri maendeleo ya elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi katika Wilaya ya Longido mkoani Arusha, huku wanafunzi wa Mpango wa Elimu kwa Waliokosa Fursa (MEMKWA) wakitajwa kuwa miongoni mwa waathirika wakubwa kutokana na mazingira magumu ya kijamii na kiuchumi.
Hali hiyo imeelezwa katika kikao cha Jukwaa la Wadau wa Elimu Wilaya ya Longido kilichoandaliwa na Shirika la Utafiti, Maendeleo na Huduma za Jamii (CORDS), kikishirikisha viongozi wa halmashauri, waratibu elimu, viongozi wa vijiji, walimu pamoja na asasi za kiraia kwa lengo la kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya elimu na kutafuta suluhisho la pamoja.
Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Elimu wa Kata ya Ngarenaibo, Paulo Teveli alisema changamoto ya wazazi kutowapelekea watoto chakula shuleni imekuwa kikwazo kikubwa kinachochangia kushuka kwa ufaulu na mahudhurio ya wanafunzi.
Alisema baadhi ya wazazi katika jamii za wafugaji bado hawajatoa kipaumbele stahiki kwa elimu, huku wengine wakikabiliwa na ugumu wa maisha unaowafanya kushindwa kuchangia mahitaji muhimu ya watoto wao shuleni.
“Tatizo hili ni kubwa na linaathiri hata wanafunzi wa MEMKWA ambao katika kata yangu wapo 31. Tunahitaji ushirikiano wa wadau wote kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia. Tunapongeza mchango wa CORDS ambao umeendelea kusaidia sekta ya elimu katika maeneo yetu,” alisema Teveli.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Longido, Sein Kitomali alisema chakula shuleni ni hitaji muhimu kwa wanafunzi wengi wanaotembea umbali mrefu kutoka makazi yao hadi shuleni.
Alisema katika jamii za kifugaji bado kuna changamoto ya baadhi ya wazazi kutothamini elimu jambo linalowafanya watoto wengi kuwa katika mazingira magumu ya kujifunza.
Kitomali alisema shule hiyo ina wanafunzi 62 wa MEMKWA, ambapo wanafunzi 38 wanatarajiwa kufanya mtihani wa darasa la nne mwaka huu.
Alieleza kuwa msaada unaotolewa na CORDS umechangia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha wanafunzi hao kuendelea na masomo kupitia upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia, sare pamoja na mahitaji mengine muhimu.
“Wanafunzi hawa wanahitaji msaada wa karibu kutokana na mazingira wanayotoka. Chakula, vifaa vya shule na mazingira bora ya kujifunzia vina mchango mkubwa katika kuongeza ari ya kujifunza,” alisema Kitomali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngoswaki, Karia Mollel alisema bado jamii nyingi za wafugaji zinakabiliwa na changamoto ya mwamko mdogo kuhusu elimu, hali inayochangia utoro na wakati mwingine ndoa za utotoni.
Alisema viongozi wa vijiji kwa kushirikiana na serikali wanaendelea kuwachukulia hatua wazazi wanaowazuia watoto kwenda shule huku kampeni za kuhamasisha uchangiaji wa chakula mashuleni zikiendelea kutolewa.
“Tunatambua elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii yetu. Tunaendelea kuwahamasisha wazazi kuhakikisha watoto wanakwenda shule na wanapata chakula ili waweze kusoma katika mazingira mazuri,” alisema Mollel.
Akizungumza kuhusu juhudi za shirika hilo, Meneja Elimu wa CORDS, Ezekiel Piniel alisema jukwaa hilo limefanyika kupitia Mradi wa Kupambana na Umasikini Kupitia Elimu na Uwezeshaji wa Kiuchumi (BELIEF), unaodhaminiwa na Shirika la Stromme Foundation.
Piniel alisema mradi huo unatekelezwa katika wilaya za Longido na Ngorongoro kwa lengo la kusaidia watoto walioko katika mazingira hatarishi kupata elimu pamoja na kuwawezesha vijana na vikundi vya kijamii kiuchumi.
Alisema kupitia mradi huo, shule za Ngoswaki na Longido zimekuwa zikinufaika kwa kupatiwa vifaa vya kujifunzia, kuboresha mazingira ya shule, kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na kutoa mafunzo mbalimbali kwa vijana.
“Mbali na kusaidia elimu, mradi huu pia unatoa mafunzo ya stadi za maisha kwa vijana kupitia programu ya Bonga na kusaidia vikundi vya ujasiriamali kujengewa uwezo wa utunzaji kumbukumbu, usimamizi wa miradi na utunzaji wa fedha,” alisema Piniel.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Nestory Dagharo alisema suala la uchangiaji wa chakula mashuleni ni muhimu na lazima kwa maendeleo ya elimu katika wilaya hiyo.
Alisema chakula kinachochangiwa na wazazi ni sehemu ya mahitaji ambayo watoto wangepata nyumbani, hivyo hakuna sababu ya wazazi kushindwa kushiriki jukumu hilo.
Aidha alisema halmashauri inaendelea kufanya vizuri katika uandikishaji wa wanafunzi kila mwaka huku jitihada za kudhibiti utoro na ndoa za utotoni zikiendelea kuzaa matunda.
“Tunashirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya elimu na mazingira bora ya kujifunzia,” alisema Dagharo.




0 Comments