MAKONDA AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUCHANGAMKIA FURSA ZA UTALII NA UWEKEZAJI TANZANIA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amewahimiza Watanzania pamoja na wawekezaji kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazozidi kujitokeza nchini, hususan katika sekta za utalii, huduma za malazi na biashara, kutokana na kuongezeka kwa mikutano na matukio makubwa ya kimataifa yanayofanyika Tanzania hususani katika jiji la Arusha.
Makonda aliyasema hayo wakati wa hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na CRDB BANK ,kwa ajili ya wanahisa waliohudhuria Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa CRDB Bank Plc, hafla iliyofanyika katika mazingira ya burudani na muziki huku zaidi ya watu 1,500 wakiwemo wanahisa, viongozi wa serikali, wafanyabiashara na wageni waalikwa wakishiriki.
Katika hafla hiyo iliyopambwa na vyakula na vinywaji vya aina mbalimbali sambamba na burudani ya muziki mzito kutoka kwa wasanii waliotumbuiza usiku kucha, Makonda alisema Tanzania inaendelea kuwa kitovu cha mikutano mikubwa ya kimataifa, jambo linalofungua milango ya fursa nyingi za uwekezaji.
Alisema ujio wa wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani unapaswa kuwa chachu kwa Watanzania kuwekeza zaidi katika hoteli, nyumba za wageni, maeneo ya burudani pamoja na huduma nyingine za kijamii na kiuchumi zitakazokidhi mahitaji ya wageni hao.
“Tunapoendelea kupokea mikutano mikubwa ya kimataifa, lazima Watanzania waone hii kama nafasi ya kujenga uchumi wao. Wageni wanapokuja nchini wanahitaji sehemu nzuri za kulala, kula, kuburudika na kupata huduma bora. Hizi zote ni fursa za uwekezaji,” alisema Makonda.
Aidha, aliipongeza CRDB Bank Plc kwa kuendelea kuwa taasisi mahiri na muhimu inayochochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia uwekezaji, utoaji wa mikopo na uwezeshaji wa sekta binafsi.
Hafla hiyo iligeuka kuwa sehemu ya kukutana kwa wadau mbalimbali wa uchumi na biashara, huku wanahisa wakitumia nafasi hiyo kujadili mustakabali wa uwekezaji na maendeleo ya benki hiyo ambayo imeendelea kuimarika ndani na nje ya Tanzania.
Mbali na chakula na vinywaji, washiriki walipata burudani ya muziki wa moja kwa moja uliowafanya wengi kusaza na kufurahia usiku huo maalum uliokuwa sehemu ya hitimisho la shughuli za mkutano mkuu wa wanahisa wa benki hiyo.
Ends

0 Comments