MAKONDA ATOA SIKU 365 KUBADILI WIZARA YA HABARI, SANAA, UTAMADUNI NA MICHEZO
Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema ndani ya mwaka mmoja Watanzania wanapaswa kuona mabadiliko makubwa katika wizara hiyo, vinginevyo yupo tayari kujiuzulu mwenyewe.
Makonda alisema dhamira yake ni kuifanya wizara hiyo kuwa kitovu cha burudani, ubunifu, ajira na furaha kwa Watanzania kupitia sekta za sanaa, michezo na utamaduni.
"Wizara yetu ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,huu ni mwezi wangu wa tatu wa kuwa waziri,Mpango wangu nikimaliza mwaka mmoja kama watanzania hamtaona mabadiliko katika ile wizara mimi najiuzulu mwenyewe"Alisema Makonda.
Akizungumza katika hafla ya chakula cha usiku kwa wanahisa wa mkutano mkuu wa 31 wa CRDB Bank Plc, Makonda alisema wizara hiyo haiwezi kuendelea kubaki ya kawaida bali lazima iwe sehemu ya kuzalisha ajira na kuondoa msongo wa mawazo kwa wananchi.
“Unaniachia eneo la utamaduni. Ulinipa uwezo wangu wa kuwa waziri. Mpango wangu ni kumaliza mwaka mmoja, kama Watanzania hamtaona mabadiliko katika wizara hiyo, mimi najiuzulu mwenyewe,” alisema Makonda.
Alisema tayari wameanza mageuzi kupitia miradi mbalimbali ikiwemo kuandaa matukio makubwa ya michezo na burudani yatakayoiweka Tanzania katika ramani ya dunia.
Makonda alisema wengi hawakuamini juhudi zao za kuwaleta mastaa wakubwa wa kimataifa nchini, lakini hatua hizo zimeanza kuzaa matunda huku akitaja kuwa nyota wa zamani wa soka la England na klabu ya Manchester United, Rio Ferdinand, anatarajiwa kuwasili nchini kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii na michezo.
Alisema kupitia wageni hao wa kimataifa, Tanzania itapata fursa kubwa ya kutangazwa duniani kutokana na mahusiano waliyonayo na mastaa na mabilionea maarufu duniani akiwemo David Beckham.
Makonda pia alisema juhudi hizo zinafanyika kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kusisitiza kufunguliwa kwa fursa za utalii, michezo na uwekezaji ili kuitangaza Tanzania kimataifa.
Aidha, alisema kulikuwa na mazungumzo yanayoendelea ya kuwashawishi mastaa wengine wakubwa duniani kuitembelea Tanzania, akimtaja nyota wa soka Cristiano Ronaldo kuwa miongoni mwa watu wanaotajwa kuonesha nia ya kuja nchini siku zijazo.
Kwa upande wake, Makonda aliwataka wadau wa CRDB Bank Plc pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana kufungua zaidi milango ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia sekta ya utalii, michezo na sanaa.
Alisema Tanzania ina kila sababu ya kuwa kivutio kikubwa duniani kutokana na rasilimali zake za utalii, utamaduni na vipaji vya vijana, huku akisisitiza kuwa wakati umefika kwa nchi kutumia nguvu ya burudani na michezo kujenga uchumi wa wananchi.
Ends..

0 Comments