KISHINDO CHA MKUTANO MKUU WA 31 WA WANAHISA WA CRDB-2026:WAPITISHA GAWIO LA SH.90 KWA HISA,

 MKUTANO MKUU WA WANAHISA WA CRDB WAPITISHA GAWIO LA SH.90 KWA HISA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MKUTANO Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa CRDB Bank Plc umepitisha kwa kishindo Ripoti ya Wakurugenzi pamoja na Taarifa za Hesabu Zilizokaguliwa kwa mwaka 2025, huku ukiidhinisha gawio la Shilingi 90 kwa kila hisa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 38 ikilinganishwa na Shilingi 65 zilizotolewa mwaka uliopita.

Mkutano huo uliofanyika leo Mei 16, 2026 jijini Arusha, pia uliidhinisha uteuzi wa Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu ya nje ya PWC kuwa wakaguzi wa hesabu za Benki kwa mwaka 2026.



Wanahisa waliohudhuria mkutano huo walieleza kuridhishwa na mwenendo wa ukuaji wa Benki hiyo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwahamasisha vijana kuwekeza katika hisa na kushiriki katika uchumi rasmi wa nchi.

Katika maazimio mengine, wanahisa walipitisha pendekezo la Mkutano Mkuu wa 32 wa Wanahisa kufanyika Mei 15, 2027 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), wakieleza kuwa vijana wengi zaidi wanapaswa kutumia fursa za uwekezaji zinazotolewa na Benki hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Plc, Dkt. Abdulmajid Mussa Nsekela, alisema mwaka 2025 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa Benki hiyo kutokana na ukuaji wa biashara, ubunifu wa kidijitali pamoja na upanuzi wa huduma zake ndani na nje ya Tanzania.

Dkt. Nsekela alisema jumla ya mali za Benki ziliongezeka kwa asilimia 33.6 na kufikia Shilingi trilioni 22.3, huku kiwango cha mikopo na advances kikifikia Shilingi trilioni 13.7.

Alisema mafanikio hayo yanaonyesha nafasi ya Benki katika kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Aidha, alisema CRDB Bank Plc itaendelea kuwekeza katika teknolojia, ujumuishaji wa kifedha na huduma zinazounganisha mifumo ya kidijitali na huduma za ana kwa ana ili kuongeza ushindani na kuboresha huduma kwa wateja.

Kwa mujibu wa Dkt. Nsekela, Benki hiyo imeendelea kupanua huduma zake kupitia mtandao wa matawi zaidi ya 261, ATM 732, mawakala 38,883 pamoja na vituo vya malipo na manunuzi 6,607 katika Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na Ofisi ya Uwakilishi ya Dubai.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Plc, Prof. Neema Mori, alisema gawio hilo la Shilingi 90 kwa kila hisa ni matokeo ya utendaji imara wa Benki hiyo pamoja na dhamira ya kuendelea kutoa thamani endelevu kwa wanahisa.

Prof. Mori alisema faida baada ya kodi kwa mwaka 2025 iliongezeka kwa asilimia 32.1 hadi kufikia Shilingi bilioni 728.6, huku mtaji wa wanahisa ukifikia Shilingi trilioni 2.7 na kiwango cha faida kwa mtaji wa wanahisa (ROAE) kufikia asilimia 29.5.

Alisema mafanikio hayo yameongeza imani ya wawekezaji na kusaidia thamani ya hisa ya Benki kufikia Shilingi 2,980 mwezi Aprili mwaka huu.

“Bodi itaendelea kusimamia ukuaji wa Benki kwa kuzingatia utawala bora, nidhamu ya kiutendaji, usimamizi madhubuti wa vihatarishi pamoja na uwekezaji katika ubunifu na teknolojia,” alisema Prof. Mori.

Naye Afisa Mkuu wa Fedha wa CRDB Bank Plc, Frederick Nshekanabo, alisema Benki hiyo imeendelea kuimarisha ufanisi wa kiutendaji kupitia usimamizi mzuri wa gharama na ukuaji wa mapato.

Alisema uwiano wa gharama dhidi ya mapato umeshuka kutoka asilimia 45.7 mwaka 2024 hadi asilimia 41.6 mwaka 2025, jambo linaloonyesha ongezeko kubwa la ufanisi wa uendeshaji.

Nshekanabo alisema mapato ya uendeshaji yaliongezeka kwa asilimia 24 hadi kufikia Shilingi trilioni 1.88, huku amana za wateja zikiongezeka kwa asilimia 36.6 hadi Shilingi trilioni 14.9.

Akifunga Mkutano Mkuu huo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Plc, Dkt. Donald Mammari, aliwashukuru wanahisa kwa ushiriki wao mkubwa na kupongeza vijana waliojitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo.

Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ilikuwa “Vijana na Uwekezaji katika Hisa.”









Ends ..

Post a Comment

0 Comments