TANROADS YAANZA KUONDOA VIBANDA,SHUGHULI ZA KIBINADAMU KWENYE HIFADHI YA BARABARA ARUSHA,MRADI MKUBWA WAANZA KUTEKELEZAA KWA KISHINDO

 TANROADS UMEANZA KUONDOA VIBANDA KWENYE HIFADHI YA BARABARA ARUSHA

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA 

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha umeanza rasmi zoezi la kuondoa vibanda, biashara na shughuli nyingine zote za kibinadamu ndani ya hifadhi ya barabara katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara ya Arusha-Kibaya-Kongwa  pamoja na kuboresha usalama katika Barabara ya Arusha Bypass.

Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Christopher Sauli amesema maandalizi yanaendelea kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya tunduzi inayounganisha maeneo ya Mbauda hadi Losinyai pamoja na kipande cha barabara ya Tipekasi kuelekea Losinyai, yenye urefu wa takribani kilomita 70.

Alisema tayari mkandarasi ameshakabidhiwa eneo la mradi huku vifaa na mitambo vikianza kufikishwa eneo la kazi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa hatua za awali za mradi huo.

“Hatua ya kwanza tunayotekeleza sasa ni kuhakikisha eneo lote la mradi linakuwa wazi ili kumpa mkandarasi nafasi ya kuanza kazi bila vikwazo vya aina yoyote,” alisema Mhandisi Sauli.

Alieleza kuwa zoezi hilo linaanza katika barabara ya Mbauda kwenda Losinyai pamoja na barabara ya Tipekasi kuelekea Losinyai, ambapo vibanda, biashara na shughuli nyingine zote zinazofanyika ndani ya hifadhi ya barabara zinaondolewa ili kupisha utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, alisema TANROADS pia inaendelea kuchukua hatua za kuboresha usalama katika Barabara ya Arusha Bypass kufuatia ongezeko la ajali zilizokuwa zikiripotiwa mara kwa mara.


Kwa mujibu wa Mhandisi Sauli, tafiti za awali zimeonesha kuwa ajali nyingi zinasababishwa na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo ya hifadhi ya barabara, hali inayochangia msongamano mkubwa wa watu na kuongeza hatari ya ajali.

“Tumeona shughuli nyingi za biashara pamoja na matumizi mengine ndani ya hifadhi ya barabara zikichangia ajali za mara kwa mara, hivyo tunaendelea kusafisha maeneo hayo ili kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara,” alisema.

Alisisitiza kuwa zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 pamoja na kanuni zake zinazokataza mtu yeyote kufanya shughuli ndani ya hifadhi ya barabara bila kibali rasmi.

Mhandisi Sauli aliongeza kuwa hatua hizo pia ni sehemu ya maandalizi ya mashindano ya michezo ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 23 yanayotarajiwa kufanyika mwaka huu, ambapo Jiji la Arusha linatarajiwa kupokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

“Tunalenga kuhakikisha Arusha inakuwa safi, salama na yenye mandhari nzuri wakati wa mashindano hayo ya kimataifa,” alisema.

Katika hatua nyingine, amewataka wakazi wa Arusha kutoa ushirikiano kwa kuondoa miundombinu na shughuli zote zilizopo ndani ya hifadhi ya barabara, ikiwemo vibanda vya biashara pamoja na miundombinu ya maji na umeme iliyopo ndani ya eneo la mradi.

Ends..

Post a Comment

0 Comments