DKT. LUKUMAY AKOSHWA NA UWEKEZAJI MKUBWA WA RAIS SAMIA SEKTA YA AFYA NCHINI

 DKT. LUKUMAY: SAMIA AWEKA MSUKUMO MKUBWA UWEKEZAJI SEKTA YA AFYA

By Arushadigital 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lukumay, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwa lengo la kuifanya Tanzania kujitegemea katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba.

Dkt. Lukumay amesema mafanikio yanayoonekana sasa katika ujenzi na uhamasishaji wa viwanda vya dawa nchini yanatokana na maelekezo na dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha Tanzania inapunguza utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje ya nchi.

Alisema mpango huo umepewa kipaumbele katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, huku Serikali ikielekeza nguvu kubwa katika kukuza viwanda vya ndani vitakavyosaidia kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wananchi.

“Binafsi ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kuwekeza katika sekta ya afya tangu alipoingia madarakani. Maelekezo yake ndiyo yamekuwa msingi wa kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini,” amesema Dkt. Lukumay.

Amesema dhamira ya Rais Samia ni kuona ifikapo mwaka 2030 Tanzania inakuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha dawa na vifaa tiba ndani ya nchi, hatua itakayosaidia wananchi kupata huduma bora za afya pamoja na kuimarisha uchumi wa taifa kupitia sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Dkt. Lukumay, Rais Samia anatamani kuona Tanzania siyo tu inajitosheleza kwa dawa na vifaa tiba, bali pia inakuwa miongoni mwa nchi zinazouza bidhaa hizo katika masoko ya kimataifa.

Alifafanua kuwa kwa sasa kiwango cha uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini bado kiko chini, ambapo Tanzania huzalisha takribani asilimia 10 pekee ya mahitaji yake, lakini Serikali imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji huo hadi kufikia kati ya asilimia 60 na 65 ifikapo mwaka 2030.

Dkt. Lukumay amesema hatua hiyo itaongeza usalama wa upatikanaji wa dawa nchini, kupunguza gharama za kuagiza bidhaa hizo kutoka nje pamoja na kufungua fursa za ajira kwa Watanzania kupitia sekta ya viwanda vya afya.

Aidha, amewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa iliyopo kuwekeza katika viwanda vya dawa na vifaa tiba, akisema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa kichocheo cha maendeleo ya taifa.

Ends..

Post a Comment

0 Comments