SERIKALI YAWATAKA WAUGUZI KUTOA HUDUMA KWA HURUMA, TANNA YAOMBA MUUNDO MPYA WA AJIRA

 SERIKALI YAWATAKA WAUGUZI KUTOA HUDUMA KWA HURUMA, TANNA YAOMBA MUUNDO MPYA WA AJIRA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


SERIKALI imewataka wauguzi na wakunga nchini kuendelea kutoa huduma za afya kwa weledi, upendo na huruma kwa wagonjwa huku Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) kikiiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa muundo mpya wa ajira kwa kada hiyo muhimu ili kuongeza morali na ufanisi katika utoaji wa huduma za afya nchini.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha Mei 12, 2026.

Akizungumza mbele ya viongozi wa Serikali, wataalamu wa afya, wadau wa maendeleo pamoja na wauguzi na wakunga kutoka maeneo mbalimbali nchini, Qwaray alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wauguzi katika kuokoa maisha ya wananchi na kuimarisha mfumo wa afya nchini.

“Akitoka Mungu, maisha ya mwanadamu yapo mikononi mwa wauguzi. Mgonjwa anapofika hospitalini, nyie ndiyo wa kwanza kumhudumia. Hatuwezi kujihudumia wenyewe tunapokuwa wagonjwa, ndiyo maana taaluma yenu ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa,” alisema Qwaray.

Hata hivyo, aliwataka baadhi ya wauguzi wanaolalamikiwa kwa kutoa huduma zisizoendana na maadili ya taaluma yao kubadilika mara moja na kurejea katika misingi ya kiapo cha uuguzi.

“Tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu baadhi ya wahudumu kuwa na nyuso za ukatili na kutumia lugha zisizofaa, hasa katika wodi za wajawazito. Mgonjwa anapokuwa hospitalini anahitaji faraja, matumaini na moyo wa upendo. Mkiwa wakali mnawaongezea maumivu,” alisema.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa wauguzi na kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi.

“Nawaomba msifanye wagonjwa wajutie kufika hospitalini. Toeni huduma kwa moyo wa huruma, utu na uzalendo kwani afya ya Watanzania inategemea huduma mnazozitoa,” aliongeza.

Aidha, Qwaray aliahidi kuwa Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyowasilishwa na wauguzi kupitia TANNA kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TANNA, Dkt. Geofrey Chacha, alisema maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani huadhimishwa kila mwaka Mei 12 kwa lengo la kutathmini huduma zinazotolewa, kuwakumbusha wauguzi maadili ya taaluma yao pamoja na kuikumbusha Serikali utekelezaji wa maazimio mbalimbali ya sekta hiyo.

Akisoma risala ya chama hicho, Dkt. Chacha alisema TANNA inaridhishwa na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya afya kupitia ujenzi wa miundombinu ya hospitali, utoaji wa ajira kwa wauguzi, upatikanaji wa vifaa tiba, uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote.

“Tunaona dhamira ya dhati ya Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya nchini. Ujenzi wa hospitali, ajira kwa wauguzi na uwekezaji wa vifaa tiba umeongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi mijini na vijijini,” alisema.

Aidha alisema kuanzia Mei 4 hadi 11, 2026, wauguzi nchini walitoa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na kufanikisha kuwafikia zaidi ya wananchi 84,149.

Kwa mujibu wa Dkt. Chacha, huduma hizo zilihusisha upimaji wa Virusi vya UKIMWI, uchunguzi wa shinikizo la damu, kisukari, saratani ya mlango wa kizazi, afya ya moyo pamoja na utoaji wa elimu ya afya ya akili.

Alisema huduma hizo ziliwezesha kubaini mapema wananchi wenye viashiria vya magonjwa mbalimbali na kuwapatia ushauri wa kitaalamu ili kuzuia madhara makubwa ya kiafya.

Katika maadhimisho hayo, TANNA pia ilisisitiza kaulimbiu ya mwaka 2026 isemayo, “Wauguzi Wetu, Mustakabali Wetu; Wauguzi Waliowezeshwa Huokoa Maisha,” ikieleza kuwa uwezeshaji wa wauguzi kupitia mafunzo, vifaa tiba na mazingira bora ya kazi ni msingi muhimu wa kuboresha huduma za afya nchini.

Dkt. Chacha alisema chama hicho kimeendelea kuimarisha taaluma ya uuguzi kupitia mafunzo endelevu ya kitaaluma (CPD), kutetea maslahi ya wauguzi, kuimarisha ushirikiano na vyama vya wauguzi vya Malawi, Zimbabwe na Rwanda pamoja na kuanzisha tuzo za kutambua wauguzi wanaofanya vizuri zaidi nchini.

Hata hivyo, TANNA ilieleza kusikitishwa na kuchelewa kwa utekelezaji wa muundo mpya wa ajira kwa wauguzi na wakunga, ikisema muundo uliopo tangu mwaka 2009 hauwatambui ipasavyo wauguzi wenye stashahada za juu, shahada za uzamili pamoja na wauguzi bingwa.

“Changamoto hii imeendelea kwa zaidi ya miaka 13 na kushusha morali ya watumishi wa kada hii muhimu katika utoaji wa huduma za afya,” alisema Dkt. Chacha.

Pia chama hicho kiligusia suala la nafasi za uongozi katika sekta ya afya, kikisema bado kuna ukosefu wa uwiano katika utoaji wa nafasi hizo kwa kada mbalimbali za wataalamu wa afya.

Kutokana na hali hiyo, TANNA iliiomba Serikali kufanya maboresho ya sera na sheria za afya ili kutoa nafasi sawa za kiuongozi kwa wataalamu wote wa afya kwa kuzingatia uwezo, elimu na uadilifu wa mhusika.

Naye Naibu Waziri anayeshughulikia masuala ya afya TAMISEMI, Jaffar Rajabu, alisema Serikali itaendelea kuongeza nguvu katika huduma za uuguzi na ukunga kwa kuhakikisha wataalamu hao wanapatiwa mazingira bora ya kazi pamoja na vifaa vya kisasa ili kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.

Maadhimisho hayo yaliwakutanisha viongozi wa Serikali, wataalamu wa afya, wadau wa maendeleo pamoja na wauguzi na wakunga kutoka maeneo mbalimbali nchini kujadili mafanikio, changamoto na mustakabali wa taaluma ya uuguzi nchini.

Ends..

Post a Comment

0 Comments