EAC YATANGAZA TUZO ZA UBORA ZA KIKANDA 2026 KUTAMBUA MAKAMPUNI BORA AFRIKA MASHARIKI

 EAC YATANGAZA TUZO ZA UBORA ZA KIKANDA 2026 KUTAMBUA MAKAMPUNI BORA AFRIKA MASHARIKI

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imetangaza rasmi Tuzo za Ubora za Kikanda za mwaka 2026 zitakazolenga kutambua na kuenzi kampuni na taasisi zinazofanya vizuri zaidi katika ukanda huo kwa kuzingatia ubora wa bidhaa na huduma, ubunifu, uzingatiaji wa viwango pamoja na maendeleo endelevu ya biashara.

Tuzo hizo zinatarajiwa kusaidia kuimarisha utamaduni wa ubora katika biashara, kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za Afrika Mashariki katika soko la kimataifa, kukuza biashara ya kikanda na kuhamasisha matumizi ya viwango vinavyotambulika kimataifa.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tuzo hizo jijini Arusha, Mkurugenzi wa Forodha wa EAC ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Flavia Busingye, alisema kuwa mashindano hayo yatafungua fursa kwa kampuni mbalimbali, hususan biashara ndogo na za kati (SMEs) pamoja na biashara zinazoongozwa na wanawake, kuonesha uwezo wao katika kutoa bidhaa na huduma zenye ubora wa hali ya juu.

Alisema EAC inaamini kuwa kupitia tuzo hizo, sekta binafsi itaendelea kuhamasika kuwekeza zaidi katika ubora, ubunifu na ushindani wa bidhaa zake katika masoko ya kikanda na kimataifa.

“Ni muhimu washindi wa tuzo hizi wakaendelea kupewa ushauri, mafunzo na ufuatiliaji ili kuwasaidia kukua na kuwa chapa imara zinazoweza kushindana kimataifa,” alisema Busingye.

Kwa mujibu wa EAC, Tuzo za Ubora za mwaka 2025 zilizofanyika jijini Nairobi, Kenya, zilivutia mashirika na kampuni 252 pamoja na washiriki zaidi ya 3,000, huku taasisi 25 zikifanikiwa kupata tuzo za kikanda kutokana na viwango vyao vya juu vya utendaji.

Katika mashindano ya mwaka 2026, kutakuwa na makundi manne ya tuzo ambayo ni Tuzo ya Bidhaa Bora ya EAC, Tuzo ya Kampuni Bora ya EAC, Tuzo za Huduma Bora pamoja na Tuzo za Wasafirishaji Bora wa Bidhaa za Kilimo Zilizoongezwa Thamani.

Makundi hayo yatashirikisha kampuni kubwa pamoja na biashara ndogo na za kati kutoka nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mashindano hayo yataanza katika ngazi za kitaifa kabla ya washindi kuingia katika hatua ya tathmini ya kikanda itakayoratibiwa na Sekretarieti ya EAC. Hafla ya utoaji wa tuzo za kikanda inatarajiwa kufanyika mjini Kigali, Rwanda, Oktoba mwaka 2026.

Mpango huo unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia Programu ya EU-EAC MARKUP II inayotekelezwa na International Trade Centre kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kikanda.






Post a Comment

0 Comments