KAMATI YA VIWANGO EAC YAENDELEA KUIMARISHA BIASHARA NA UBORA WA BIDHAA KIKANDA

 KAMATI YA VIWANGO EAC YAENDELEA KUIMARISHA BIASHARA NA UBORA WA BIDHAA KIKANDA

Na Joseph Ngilisho – Arusha

KAMATI ya Viwango ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika masuala ya uandaaji wa viwango, ukaguzi wa ubora wa bidhaa, vipimo na uthibitishaji kupitia Mkutano wake wa 28 unaoendelea kufanyika jijini Arusha.

Mkutano huo unaofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanzia Mei 12 hadi 14, 2026, umewakutanisha wataalamu kutoka nchi wanachama wa EAC, kamati ndogo za kitaalamu, taasisi za viwango pamoja na washirika wa maendeleo kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha biashara ndani ya ukanda huo.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mwakilishi wa Shirika la Viwango Tanzania, David Lema, alisema kamati hiyo ni chombo cha kisheria kilichoanzishwa chini ya sheria za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kuratibu na kufuatilia shughuli za viwango, ukaguzi wa ubora, vipimo pamoja na uthibitishaji wa bidhaa na huduma.

Alisema lengo kuu la kamati hiyo ni kuhakikisha biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inaendelea kukua kwa kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi vinavyoweza kuchelewesha usafirishaji wa bidhaa na huduma kati ya nchi wanachama.

“Tunataka kuwa na mfumo mmoja wa viwango utakaorahisisha biashara, kuongeza ushindani wa bidhaa za Afrika Mashariki na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa katika ukanda wetu zinakidhi ubora unaokubalika kimataifa,” alisema Lema.

Aliongeza kuwa mkutano huo pia umejadili maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya viwango na ubora, pamoja na kuweka vipaumbele vya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa lengo la kuimarisha sekta ya viwanda na biashara ndani ya EAC.

Kwa mujibu wa Lema, ushirikiano huo wa kikanda utasaidia kuongeza ufanisi wa mifumo ya vipimo na uthibitishaji wa bidhaa, kulinda afya na usalama wa walaji, pamoja na kufungua fursa zaidi za biashara ndani na nje ya Afrika Mashariki.

Mkutano huo unatajwa kuwa sehemu ya jitihada za Jumuiya ya Afrika Mashariki za kuimarisha mtangamano wa kiuchumi kwa kutumia viwango vya pamoja vitakavyosaidia kukuza ushindani wa bidhaa na huduma katika soko la kikanda na kimataifa.






Post a Comment

0 Comments