JIJI LA ARUSHA LAZINDUA HOSPITALI YA PILI YA WILAYA, KALOLENI YAPANDISHWA HADHI
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
JIJI la Arusha limezindua hospitali yake ya pili ya wilaya baada ya kupandishwa hadhi kwa iliyokuwa Kituo cha Afya Kaloleni kuwa Hospitali ya Wilaya ya Arusha, hatua inayolenga kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi na kupunguza msongamano katika hospitali kubwa za rufaa.
Uzinduzi huo uliambatana na zoezi la upimaji wa magonjwa mbalimbali pamoja na utoaji wa matibabu bure kwa wakazi wa Jiji la Arusha kwa muda wa siku mbili.
Akizungumza katika hafla hiyo leo May 5,2026, Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Jacob Rombo, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, alisema mafanikio ya hospitali hiyo yatategemea ushirikiano wa wananchi wote katika kuitunza, kuilinda na kuhakikisha vifaa pamoja na huduma zilizowekwa zinawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.
Alisema hospitali hiyo ni mali ya umma iliyojengwa kwa fedha za walipa kodi, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha mali zote zilizopo zinatunzwa na kulindwa dhidi ya ubadhirifu.
“Hospitali hii ni mali ya wananchi wote. Tusione jukumu la kuitunza ni la walinzi au viongozi pekee. Kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha vifaa, dawa na mazingira ya hospitali vinabaki salama kwa manufaa ya jamii,” alisema Rombo.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi au uongozi wa hospitali wanapoona vitendo vya wizi, uharibifu wa vifaa tiba au matumizi mabaya ya mali za umma.
Aidha, aliwahimiza wananchi kutumia huduma zinazotolewa hospitalini hapo, kuzingatia usafi wa mazingira pamoja na kujiunga na mifumo ya bima ya afya ili kurahisisha upatikanaji wa matibabu.
Kwa upande wa watumishi wa afya, aliwataka kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na moyo wa huruma kwa wananchi, akisisitiza kuwa afya bora ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Katika hotuba hiyo, Rombo pia aliwahimiza wanawake wajawazito kuacha tabia ya kujifungulia majumbani na badala yake kutumia vituo vya afya na hospitali kwa ajili ya huduma salama za uzazi.
“Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha kina mama wanajifungua salama katika vituo vya afya vyenye wataalamu na vifaa tiba vya kisasa. Tuachane na kujifungulia nyumbani au kwenda kwa waganga wa kienyeji,” alisema.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Shaban Manyama, alisema Halmashauri ya Jiji la Arusha imeweka mkakati wa kuwa na hospitali tatu za wilaya kwa lengo la kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi.
Manyama alisema kwa sasa tayari jiji hilo lina hospitali mbili za wilaya ambazo ni Hospitali ya Wilaya ya Njiro pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Kaloleni iliyozinduliwa rasmi, huku juhudi zikiendelea kuhakikisha hospitali hizo zinaimarishwa kwa vifaa tiba vya kisasa pamoja na wataalamu wa afya wa kutosha.
“Tunalenga kuhakikisha wananchi wa Arusha hawalazimiki kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya. Ndiyo maana tunaendelea kuboresha miundombinu ya hospitali, kuongeza vifaa tiba pamoja na watumishi wa afya ili huduma ziwe bora zaidi,” alisema Manyama.
Aidha, alisema kupandishwa hadhi kwa Kituo cha Afya Kaloleni kuwa Hospitali ya Wilaya ni hatua kubwa katika kuimarisha huduma za afya jijini humo, kwani itaongeza uwezo wa kutoa huduma mbalimbali za kibingwa ambazo hapo awali zilikuwa zinapatikana katika hospitali kubwa pekee.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Willfred Soilel, aliutaka uongozi wa hospitali zote jijini humo kuhakikisha unatanguliza utoaji wa huduma kwa wagonjwa badala ya kuweka mbele malipo, ili kuokoa maisha ya wananchi na kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika.
Soilel alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kucheleweshewa huduma kutokana na taratibu za malipo, hali ambayo wakati mwingine huweka maisha ya wagonjwa katika hatari.
“Huduma kwa mgonjwa inapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza. Tusikimbilie malipo kabla ya kuokoa maisha ya watu. Wananchi wanapofika hospitalini wanahitaji kupewa huduma kwa wakati ili kuepusha madhara makubwa zaidi,” alisema Soilel.
Kwa upande wake, Rombo alisema Serikali ya Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha sekta ya afya kwa kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi pamoja na kuongeza uwekezaji katika vifaa tiba na rasilimali watu.
Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Arusha katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, akieleza kuwa fedha zinazokusanywa kupitia kodi na ushuru ndizo zinazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama hospitali hiyo.
“Wananchi wasiwaone watumishi wa mapato kama maadui. Fedha hizi ndizo zinazorudi kwa wananchi kupitia huduma za afya, elimu na maendeleo mengine muhimu,” alisema.
Hafla hiyo iliambatana na maandamano ya watumishi wa jiji na wauguzi kutoka ofisi ya Mkuu WA wilaya hadi katika hospitali hiyo na zoezi maalumu la upimaji wa magonjwa mbalimbali pamoja na utoaji wa matibabu bure kwa wakazi wa Jiji la Arusha, ambapo wananchi wengi walijitokeza kupata huduma hizo.
ENDS.









0 Comments