MFANYABIASHARA ARUSHA AFIA KWA SANGOMA ,MWILI WAKUTWA UMEHARIBIKA VIBAYA SANGOMA APIGA KOFURI NYUMBA NA ASEPA HARUFU YAWASHTUA MAJIRANI

 Mfanyabiashara Afia Kwa Sangoma, Mwili Wake Wakutwa Umeharibika Arusha

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

SIMANZI na taharuki vimetawala familia ya mfanyabiashara Sifaeli Mollel baada ya mwili wake kukutwa ukiwa umeharibika ndani ya nyumba inayodaiwa kutumiwa na mganga wa jadi katika eneo la Muriet, jijini Arusha.

Mollel (48), mkazi wa Kijenge katika Kata ya Kimandolu, alidaiwa kutoweka Mei 3, 2026 katika mazingira ya kutatanisha kabla ya mwili wake kupatikana siku saba baadaye, tukio lililoibua hofu kubwa kwa familia, majirani na wakazi wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, mazingira ya tukio hilo yamejaa mashaka makubwa kutokana na kuwepo kwa vitu vinavyodaiwa kutumika katika tiba za jadi pamoja na vitambulisho vyenye majina tofauti vilivyokutwa ndani ya nyumba hiyo.

Familia hiyo imeliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa tukio hilo na kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuhusika.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha kifo hicho pamoja na watu wote waliohusika.

Alisema polisi tayari wameanza kuchukua hatua mbalimbali za kiuchunguzi na kwamba taarifa kamili zitatolewa mara baada ya uchunguzi kukamilika.

“Tunaendelea na uchunguzi wa tukio hili na tutahakikisha sheria inachukua mkondo wake dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika,” alisema Kamanda Masejo.

Tukio hilo limewaacha wakazi wa Muriet na maeneo jirani wakiwa na maswali mengi kuhusu mazingira ya kutoweka kwa mfanyabiashara huyo na namna mwili wake ulivyopatikana ndani ya nyumba hiyo inayohusishwa na shughuli za uganga wa jadi.

Ends..

Post a Comment

0 Comments