KARIBU-KILIFAIR 2026 YAJA KIVINGINE ARUSHA YAPANUA MAONESHO, WAONESHAJI 550 KUSHIRIKI

KARIBU-KILIFAIR 2026 KUNG’ARA ARUSHA, KUIFANYA TANZANIA KITOVU CHA UTALII AFRIKA MASHARIKI

Na Joseph Ngilisho – Arusha

JIJI la Arusha linatarajiwa kuwa mwenyeji wa maonesho makubwa zaidi ya utalii Afrika Mashariki, ya KARIBU-KILIFAIR 2026, yatakayowakutanisha maelfu ya wadau wa sekta ya utalii, wawekezaji, mawakala wa safari na viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Maonesho hayo ambayo yameendelea kujijengea heshima kimataifa, yanatajwa kuwa lango kuu la biashara ya utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara, huku yakiiweka Tanzania katika nafasi muhimu ya ushindani wa soko la utalii duniani .

Maonesho hayo yanatarajiwa kufunguliwa June 4-7,2026  na waziri wa maliasili na utalii,DKT ASHATU KIKAJI pamoja na waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo,Paul Makonda Katika viwanja vya Magereza Kisongo Arusha.

KARIBU-KILIFAIR ilianzishwa baada ya kuunganishwa kwa maonesho mawili makubwa ya utalii nchini, ambayo ni KARIBU Fair ya Chama cha Waendeshaji wa Utalii Tanzania (TATO) pamoja na KILIFAIR ya kampuni ya Kilifair Promotion, hatua iliyosaidia kuunda jukwaa kubwa zaidi la biashara ya utalii katika ukanda huu.

Kwa mwaka 2026, waandaaji wa maonesho hayo wametangaza kuwa tukio hilo litafanyika kwa siku nne mfululizo, tofauti na miaka iliyopita, huku likipanuliwa kufikia eneo la maonesho lenye ukubwa wa mita za mraba 47,000.

Zaidi ya waoneshaji 550 kutoka mataifa 14 wanatarajiwa kushiriki, sambamba na mawakala na waendeshaji wa safari zaidi ya 1,000 kutoka nchi zaidi ya 40 duniani. Aidha, zaidi ya wageni na wadau wa utalii 15,000 wanatarajiwa kuhudhuria maonesho hayo.

Wakurugenzi wa KILIFAIR Promotion Co. Ltd, Tom Kunkler na Dominic Shoo,wakiongea na waandishi wa habari May 14,2026 , wamesema maonesho ya mwaka huu yataendelea kujikita katika viwango vya kimataifa, ubunifu na utoaji wa fursa za biashara kwa wadau wa utalii.

Kwa mujibu wa waandaaji hao, mwaka huu kutakuwa na maeneo mapya ya maonesho yakiwemo “Pan Africa Pavilion” chini ya kampeni ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya “Visit East Africa – Feel the Vibe”, inayolenga kutangaza vivutio vya utalii, tamaduni na fursa za uwekezaji zilizopo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Kaulimbiu yetu ya ‘Where business meets wildlife’ inaendelea kuonesha namna Tanzania ilivyo mahali sahihi pa kuunganisha biashara, mikutano na utalii wa wanyamapori,” walisema waandaaji hao.

Walieleza kuwa Tanzania imeendelea kuwa moja ya nchi zinazoongoza kwa utalii wa mikutano na biashara (MICE), kutokana na mazingira yake ya kipekee yanayounganisha shughuli za biashara na vivutio vya asili vinavyovutia watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Waandaaji hao pia waliishukuru Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya utalii nchini, pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii, Waziri wa Maliasili na Utalii Ashatu Kijaji, Tanzania Tourist Board (TTB), Tanzania National Parks Authority (TANAPA) na wadau wengine wa sekta hiyo.

Mbali na maonesho hayo, Tanzania imeendelea kujivunia kuwa moja ya nchi zenye utajiri mkubwa wa rasilimali za utalii duniani. Nchi ina ukubwa wa kilomita za mraba 945,234 ambapo zaidi ya asilimia 32 ya eneo lote ni maeneo yaliyohifadhiwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Maeneo hayo yanajumuisha hifadhi za taifa 21, mapori ya akiba 29, eneo la hifadhi ya Ngorongoro Conservation Area, pamoja na maeneo mbalimbali ya urithi wa utamaduni, misitu ya asili na hifadhi za mazingira.

Miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii vinavyoendelea kuitangaza Tanzania duniani ni Serengeti National Park, kreta ya Ngorongoro Crater na Mount Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu zaidi barani Afrika.

Vivutio vingine ni pamoja na Mikumi National Park, Ruaha National Park pamoja na Selous Game Reserve, sambamba na fukwe za Bahari ya Hindi zinazopatikana katika maeneo mbalimbali ya pwani ya Tanzania.

Kupitia KARIBU-KILIFAIR 2026, Tanzania inatarajiwa kuendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha utalii, biashara na uwekezaji barani Afrika huku Arusha ikiendelea kuwa moyo wa sekta ya utalii nchini.





Ends 

Post a Comment

0 Comments