KISHINDO CHA CRDB BANK YAPATA FAIDA YA SHILINGI BILIONI 206, YAONGEZA GAWIO KWA WANAHISA,KUFANYA MKUTANO MKUU WA 31 ARUSHA

 CRDB YAPATA FAIDA YA SHILINGI BILIONI 206, YAONGEZA GAWIO KWA WANAHISA,KUFANYA MKUTANO MKUU WA 31 ARUSHA

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

BENKI ya CRDB imeendelea kuandika historia mpya katika sekta ya fedha nchini baada ya kutangaza faida ya zaidi ya Shilingi bilioni 206 sambamba na kuongeza gawio kwa wanahisa wake kutoka Shilingi 65 hadi Shilingi 90 kwa kila hisa, hatua inayoonesha uimara mkubwa wa kifedha na ukuaji endelevu wa taasisi hiyo.

Mafanikio hayo yameelezwa jijini Arusha na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Plc, Profesa Neema Mori pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dkt. Abdulmajid Nsekela, wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuelekea Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa CRDB utakaofanyika Mei 16, 2026 katika Ukumbi wa Simba uliopo ndani ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Mkutano huo utatanguliwa na semina maalumu ya wanahisa itakayofanyika Mei 15, 2026 ikiwa imeboreshwa na kupewa hadhi ya “Siku ya Wawekezaji”, huku Waziri wa Fedha, Hamis Omari akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya benki hiyo,May 13,2026 Dkt. Nsekela alisema CRDB imeendelea kuimarika kiutendaji na kifedha kutokana na imani kubwa ya wateja, wanahisa pamoja na uwekezaji mkubwa katika teknolojia na ubunifu wa huduma za kifedha.

Faida ya zaidi ya Shilingi bilioni 206 si jambo dogo katika sekta ya fedha. Hii ni ishara ya kuaminika kwa benki yetu, uimara wa mifumo yetu na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wanahisa, wateja na wadau wetu,” alisema Dkt. Nsekela.

Alisema CRDB imeendelea kuwa kinara wa sekta ya benki nchini kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia huduma za kisasa za kidijitali na mifumo bunifu ya kifedha inayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja.

Kwa upande wake, Profesa Mori alisema mafanikio hayo yameiwezesha benki hiyo kuongeza kiwango cha gawio kwa wanahisa wake, hatua inayodhihirisha namna taasisi hiyo inavyoendelea kukua na kutoa thamani kwa wawekezaji wake.

Hili ni ongezeko muhimu ambalo linaonyesha namna benki yetu inavyoendelea kufanya vizuri na kuwajali wanahisa wake.

 Tunawashukuru wanahisa wote kwa kuendelea kutuamini na kushirikiana nasi katika safari ya ukuaji wa benki yetu,” alisema Profesa Mori

Alieleza kuwa CRDB ni miongoni mwa taasisi chache zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), jambo ambalo limeiwezesha kuvutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya Tanzania huku ikiongeza ushiriki wa wananchi katika uwekezaji wa hisa.

Aidha, viongozi hao walisisitiza kuwa vijana ni nguvu kubwa ya ukuaji wa uchumi wa sasa na wa baadaye, hali iliyosababisha kaulimbiu ya mwaka huu kuwa “Vijana na Uwekezaji katika Hisa”.

Profesa Mori alisema semina ya mwaka huu inalenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu uwekezaji katika masoko ya mitaji, matumizi sahihi ya huduma za kifedha pamoja na namna ya kujenga uhuru wa kifedha kupitia uwekezaji halali.

Vijana ndio nguvu kubwa ya uchumi wetu. Wana ubunifu, ari na uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa, lakini bado wengi hawajapata elimu ya kutosha kuhusu uwekezaji katika hisa.

 Kupitia semina hii tunataka kufungua macho yao kuhusu fursa zilizopo,” alisema.

Katika hatua nyingine CRDB  imezindua rasmi Ripoti ya Mwaka 2025 katika mkutano huo na waandishi wa habari.

Ripoti hiyo imeeleza kwa kina utendaji wa benki, mafanikio yaliyopatikana, pamoja na hatua mbalimbali za ukuaji wa biashara na uendelevu zilizotekelezwa katika mwaka uliopita.

Naye Dkt. Nsekela alisema haiwezekani kuzungumzia mustakabali wa taasisi ya kifedha bila kuwatazama vijana kwani ndio wawekezaji, wabunifu na viongozi wa kesho watakaoibeba CRDB katika miaka ijayo.

Hawa ndio wateja, wabunifu, wawekezaji na viongozi wa kesho. Tunataka kuwawezesha zaidi katika matumizi ya teknolojia, huduma za kifedha na uwekezaji ili washiriki kikamilifu katika uchumi wa taifa,” alisema.

Aliongeza kuwa benki hiyo sasa inaingia katika awamu mpya ya ukuaji ikiwa na maono ya kupanua huduma zake ndani na nje ya Tanzania sambamba na kuendelea kuboresha mifumo ya kidijitali ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wateja na wanahisa.


Profesa Mori alisema mkutano mkuu wa mwaka huu utaendeshwa kwa mfumo wa mseto (hybrid), ambapo baadhi ya wanahisa watashiriki ukumbini huku wengine wakifuatilia kwa njia ya mtandao, hatua inayolenga kuongeza ushiriki mpana zaidi wa wanahisa kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Alisema CRDB imeendelea kufanya maboresho ya kidijitali kupitia huduma mbalimbali ikiwemo SimBanking ili kuhakikisha wanahisa wanapata urahisi wa kushiriki mkutano huo na kupata taarifa muhimu kwa wakati.










Post a Comment

0 Comments