POLISI DODOMA WAWAKAMATA KAHABA 39 KWA TUHUMA ZA KUJIUZA, WADAIWA KUWASUMBUA WABUNGE
Na Arushadigital |DODOMA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limefanikiwa kuwakamata watu 39 wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara haramu ya ukahaba katika operesheni maalumu iliyotekelezwa kwa kipindi cha karibu mwezi mmoja ndani ya Jiji la Dodoma.
Operesheni hiyo iliyoanza Aprili 14 na kuhitimishwa Mei 11, 2026, imelenga kudhibiti vitendo vinavyokiuka maadili ya jamii pamoja na kuimarisha usalama katika maeneo mbalimbali ya makao makuu ya nchi, hususan maeneo yanayozunguka taasisi za Serikali na shughuli za Bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti yaliyokuwa yakitajwa kuwa vinara wa vitendo hivyo.Kamanda Hyera amesema baadhi ya watuhumiwa wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya usumbufu kwa wabunge na viongozi wengine wanaotekeleza majukumu yao ya kiserikali, jambo ambalo limechochea Jeshi la Polisi kuongeza nguvu katika operesheni hizo.
“Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili, sheria na utulivu wa jamii, hasa katika Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi,” amesema Kamanda Hyera.
Aidha, amesema uchunguzi dhidi ya watuhumiwa hao unaendelea huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa mara baada ya taratibu kukamilika.
Jeshi hilo limeeleza kuwa oparesheni hiyo ni endelevu na inalenga kurejesha nidhamu, usalama na utulivu katika maeneo ya umma ambayo yamekuwa yakitumika kwa shughuli zinazokiuka sheria.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kushirikiana kwa kutoa taarifa za uhalifu na vitendo vinavyohatarisha maadili na amani ya jamii ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.



0 Comments