PBZ BANK YAPANUA HUDUMA YATINGA ARUSHA KWA KISHINDO,NAIBU WAZIRI AZINDUA TAWI AHIMIZA MATUMIZI YA MIKOPO NAFUU KUCHOCHEA UWEKEZAJI

  NAIBU WAZIRI AHIMIZA MATUMIZI YA MIKOPO NAFUU, PBZ YAPANUA HUDUMA ARUSHA

.....Yalenga kuchochea uwekezaji, kukuza ushindani na kufungua fursa mpya za kiuchumi

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA 


NAIBU Waziri katika Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Stephen Chaya, amewataka wafanyabiashara nchini kutumia kikamilifu fursa za kifedha zinazotolewa na benki zenye riba nafuu ili kuongeza kasi ya uwekezaji na kukuza ushindani wa biashara.

Akizungumza jijini Arusha katika hafla ya uzinduzi wa tawi jipya la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ Bank), Dkt. Chaya alisema upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu ni nyenzo muhimu kwa wafanyabiashara kukuza mitaji na kupanua shughuli zao za kiuchumi.


Alisema taasisi za kifedha zina wajibu wa kubuni huduma zinazozingatia mahitaji halisi ya wananchi ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa taifa.

“Tunataka kuona wafanyabiashara wanapata mikopo kwa urahisi na kwa masharti rafiki ili waweze kuwekeza zaidi na kuongeza tija katika biashara zao,” alisisitiza.

Dkt. Chaya aliitaja PBZ kuwa miongoni mwa benki zinazotoa huduma rafiki kwa wateja, akieleza kuwa ushindani unaoletwa na taasisi kama hiyo unachochea ubunifu na upatikanaji mpana wa huduma za kifedha nchini.

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza upatikanaji wa mitaji na kuimarisha mifumo ya kifedha ili kuwezesha sekta binafsi kuwa injini ya uchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa PBZ Bank, CPA Fahad Soud Hamid, alisema benki hiyo inaendelea kupanua mtandao wake wa huduma nchini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kusogeza huduma karibu na wananchi.

Alisema PBZ, iliyoanzishwa mwaka 1966 na inayokaribia kutimiza miaka 60, imejijengea nafasi imara kama moja ya benki kongwe na yenye ushindani nchini, huku ikiwa na matawi na vituo vya huduma zaidi ya 20 pamoja na mawakala zaidi ya 1,200.

“PBZ si benki ya Zanzibar pekee, bali ni benki ya Watanzania wote. Tupo hapa Arusha kusogeza huduma karibu zaidi na wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla,” alisema.

Alieleza kuwa benki hiyo inatoa huduma mbalimbali ikiwemo akaunti za akiba, biashara, uwekezaji na mikopo kwa wateja binafsi na wafanyabiashara, pamoja na huduma za benki ya Kiislamu zinazotoa mikopo isiyo na riba.

Kwa mujibu wa CPA Hamid, PBZ imefikia rasilimali zinazozidi shilingi trilioni 3, huku kiwango cha mikopo chechefu kikiwa chini ya asilimia 2—chini ya kiwango kinachoruhusiwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Aidha, alisema benki hiyo ina uwezo wa kutoa mikopo mikubwa hadi dola milioni 25 kwa mkupuo mmoja, hatua inayolenga kusaidia uwekezaji mkubwa na kukuza biashara nchini.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, alisema ujio wa PBZ katika jiji hilo ni chachu ya ukuaji wa uchumi, akibainisha kuwa takribani asilimia 85 ya wakazi wa Arusha wanajihusisha na shughuli za biashara.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022, Mkoa wa Arusha una zaidi ya wakazi milioni 2.6, hali inayoongeza uhitaji wa huduma za kifedha ili kusaidia ukuaji wa biashara na uwekezaji.

“Uwepo wa benki hii utaongeza ushindani katika sekta ya fedha, kuboresha huduma na kufungua fursa za ajira kwa vijana,” alisema Mkude.

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege pamoja na maandalizi ya michuano ya AFCON, hatua zitakazoongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Mkude pia alihimiza wananchi kulipa kodi na kudai risiti za kielektroniki (EFD) ili kuongeza mapato ya serikali kwa maendeleo ya huduma za kijamii.

Ufunguzi wa tawi la PBZ Arusha unatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha katika Kanda ya Kaskazini, huku ukiwa chachu ya kukuza biashara, uwekezaji na uchumi wa wananchi kwa ujumla


Ends ..

Post a Comment

0 Comments