NCHIMBI AFUNGUA MKUTANO MKUBWA WA TAPSEA ARUSHA,MWENYEKITI WAANDISHI NA WAENDESHA OFISI KUDHALILISHWA MITANDAONI

 SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MASLAHI YA WATUMISHI, KUONGEZA AJIRA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma nchini huku ikisisitiza uwajibikaji, maadili na weledi katika utendaji kazi.

Dkt. Nchimbi aliyasema hayo May 21,2026 wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama cha Waandishi na Waendesha Ofisi Tanzania Bara na Zanzibar (TAPSEA) uliofanyika katika hotel ya Ngurdoto Mountain Lodge iliyopo nje kidogo ya jiji la Arusha  na kuhudhuriwa na zaidi ya wajumbe 5,000 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema maendeleo ya taifa yanategemea mchango mkubwa wa watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa uaminifu, uzalendo na nidhamu huku akiwataka watumishi kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kitaaluma ili kujenga uwezo na kuongeza ufanisi katika kazi.

“Mtumishi anayeshiriki katika shughuli za taasisi huonyesha uwajibikaji na dhamira ya kweli ya kulitumikia taifa,” alisema Dkt. Nchimbi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, alisema serikali itaendelea kuajiri watumishi wapya na kuboresha maslahi yao ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.

Alisema katika bajeti ya mwaka 2025/2026 serikali iliidhinisha ajira mpya 42,500, kupandisha vyeo watumishi wa umma 219,042 na kuwabadilishia muundo watumishi 6,198, huku watumishi 18,830 wakilipwa malimbikizo ya mishahara yao.

Kikwete alisema katika mwaka wa fedha 2026/2027 serikali imepanga kuajiri watumishi wapya 45,000 wa kada mbalimbali ikiwemo kada ya waandishi na waendesha ofisi pamoja na kuwapandisha madaraja watumishi 234,221.

“Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao kwa wakati,” alisema Kikwete.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mwl.Haroun Ali Suleiman, aliipongeza TAPSEA kwa kuendelea kuimarisha mshikamano wa Muungano kupitia ushirikiano wa wanachama kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema chama hicho kimeendelea kuwa mfano wa umoja kwa kuwakutanisha wataalamu kutoka pande zote mbili za Muungano na kuimarisha mahusiano ya kitaaluma.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa TAPSEA, Zuhura Maganga, alikemea vitendo vya kudhalilisha kada ya waandishi na waendesha ofisi kupitia mitandao ya kijamii akisema vinaendelea kushusha hadhi ya taaluma hiyo muhimu katika utumishi wa umma.

“Hii ni kada ya kitaaluma yenye maadili, nidhamu na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa. Hatutakubali kada yetu kudhalilishwa,” alisema Maganga.

Alisema waandishi na waendesha ofisi wamekuwa wakifanya kazi kubwa katika uratibu wa shughuli za viongozi, usimamizi wa taarifa na mawasiliano ya taasisi mbalimbali nchini.

Aidha, alisema TAPSEA inaendelea kujiimarisha kiuchumi kupitia uwekezaji wa mali za chama ambapo tayari kimefanikiwa kupata viwanja viwili kwa ajili ya kujenga ofisi za kudumu pamoja na vitega uchumi.

Mkutano huo wa siku kadhaa unatarajiwa kujadili maendeleo ya taaluma ya waandishi na waendesha ofisi, matumizi ya teknolojia katika utendaji kazi pamoja na mbinu za kuongeza ufanisi katika taasisi za umma na binafsi.














Ends..

Post a Comment

0 Comments