DKT LUKUMAY ATOA WITO WA HATUA ZA HARAKA KUTOKOMEZA HOMA YA INI DUNIANI
By Joseph Ngilisho-Arushadigital
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Johannes Lukumay, alisema dunia inapaswa kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya homa ya ini ya virusi ili kuokoa mamilioni ya maisha na kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Dkt. Lukumay ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, alisema hayo katika mkutano wa pembeni wa Mkutano Mkuu wa 79 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaofanyika nchini Uswisi, uliojadili namna ya kuimarisha juhudi za kutokomeza homa ya ini kama tishio kwa afya ya umma.
Alisema homa ya ini ni miongoni mwa magonjwa ya kuambukiza yanayoongoza kwa kusababisha vifo duniani, huku zaidi ya watu milioni 1.3 wakifariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huo ambao unaweza kuzuilika na kutibika.
Kwa mujibu wa Dkt. Lukumay, takribani watu milioni 300 duniani wanaishi na virusi vya homa ya ini aina ya B au C, hali inayohitaji hatua za haraka na uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya.
“Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa licha ya homa ya ini kuzuilika, kutibika na hata kupona kupitia hatua madhubuti za afya ya umma, bado saratani ya ini na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo vinaendelea kuongezeka,” alisema.
Aidha, alisema nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani zinapaswa kuthibitisha upya dhamira yao ya pamoja ya kutokomeza maambukizi ya homa ya ini pamoja na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Dkt. Lukumay alisema bado homa ya ini haijapewa kipaumbele cha kutosha katika ajenda ya afya duniani licha ya kuwepo kwa mkakati wa Shirika la Afya Duniani wa miaka 2022 hadi 2030 unaolenga kutokomeza ugonjwa huo.
Alisema hatua za haraka, uwekezaji mkubwa na utekelezaji madhubuti wa mipango ya afya vinahitajika ili kufikia malengo ya kutokomeza homa ya ini na kupunguza mzigo wa magonjwa ya ini pamoja na saratani ya ini.
Katika hatua nyingine, alizipongeza nchi zilizoanzisha programu madhubuti za mapambano dhidi ya homa ya ini, akisema zimeonyesha kuwa inawezekana kutokomeza ugonjwa huo kupitia uongozi wa kisiasa wenye msimamo, huduma sawa kwa wananchi wote na kuzingatia haki za binadamu.
Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto kubwa katika uchunguzi, matibabu na upatikanaji wa fedha za kufadhili mapambano dhidi ya homa ya ini.
“Ni lazima kuwe na uwekezaji mkubwa katika huduma za kinga, uchunguzi na matibabu bila ubaguzi wala unyanyapaa, sambamba na kuimarisha teknolojia na uzalishaji wa dawa ndani ya nchi,” alisema.
Pia alisema kuna umuhimu wa kuunganisha huduma za matibabu ya homa ya ini katika mfumo wa huduma za afya kwa wote pamoja na huduma za msingi za afya ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, hasa makundi yaliyo hatarini.
Kwa mujibu wa Dkt. Lukumay, mabadiliko katika mfumo wa ufadhili wa afya duniani yanapaswa kuifanya kila nchi kuongeza umiliki wa ndani na kutenga rasilimali zake kusaidia kutokomeza homa ya ini huku ikiendelea kushirikiana na wadau wa kimataifa.
Alisema mafanikio ya kutokomeza homa ya ini yanaweza kuzuia maambukizi mapya milioni 36, kuokoa maisha ya watu milioni 10 na kuongeza uzalishaji wa kiuchumi duniani kwa dola bilioni 145.
Kadhalika, alisema kuna haja ya kuharakisha tafiti na ubunifu wa teknolojia mpya za kugundua na kutibu homa ya ini ya virusi, hasa homa ya ini aina ya B pamoja na maambukizi yanayoambatana na homa ya ini Delta.
Dkt. Lukumay pia alisema kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, asasi za kiraia, mashirika yanayoongozwa na wagonjwa pamoja na mitandao ya kijamii katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Aidha, alisema dunia inapaswa kuungana kuunga mkono azimio la Mkutano wa Shirika la Afya Duniani wa mwaka 2027 litakalolenga kuongeza kasi ya maendeleo ya kimataifa na kuhuisha dhamira za kitaifa na kimataifa za kutokomeza homa ya ini.
Alisema hatua hiyo itaweka msingi wa kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu homa ya ini ifikapo mwaka 2028 ili kuimarisha zaidi mapambano ya kimataifa dhidi ya ugonjwa huo.
Ends..


0 Comments