MZUMBE YAZINDUA PROGRAMU ZA UTALII NA KILIMO TANGA, YAFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI
Na Hadija Bagasha | Tanga
Chuo Kikuu cha Mzumbe kimejipanga kuwa chachu ya mapinduzi ya sekta za utalii na kilimo nchini baada ya kuzindua programu mpya za elimu katika Kampasi yake ya Tanga, hatua inayolenga kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kisasa huku ikifungua fursa mpya za uwekezaji katika Mkoa wa Tanga.
Uzinduzi huo umetangazwa katika Maonyesho ya 13 ya Biashara na Utalii yanayoendelea jijini Tanga, ambapo viongozi wa chuo hicho wamesema kuwa programu hizo za ngazi ya cheti na stashahada zimeandaliwa mahsusi kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia ukuaji wa sekta zinazobeba uchumi wa taifa.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Felchesmi Lyakurwa, alisema Tanzania inahitaji wataalamu wengi zaidi katika sekta za utalii na kilimo ili kuongeza tija, ushindani na mchango wa sekta hizo katika maendeleo ya uchumi.
“Tunahitaji wataalamu wengi zaidi katika sekta za utalii na kilimo ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa kisasa. Kupitia programu hizi mpya, Chuo Kikuu Mzumbe kitachangia kuzalisha vijana wabobezi watakaoongeza tija katika sekta hizo muhimu kwa taifa,” alisema Dk. Lyakurwa.
Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii vinavyovutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi, huku Mkoa wa Tanga ukiwa miongoni mwa maeneo yenye hazina kubwa ya vivutio ambavyo bado havijatumika kikamilifu kutokana na uhaba wa wataalamu wa kutosha katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wake, programu hizo zitawajengea wanafunzi uwezo katika usimamizi wa utalii, huduma kwa wageni, uhifadhi wa mazingira na matumizi ya teknolojia za kisasa katika kukuza utalii endelevu.
Katika sekta ya kilimo, alisema mafunzo yatakayokuwa yakitolewa yatawapa vijana maarifa na stadi za kisasa zitakazowawezesha kuendesha kilimo chenye tija, kuongeza uzalishaji na kutumia teknolojia zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na la kimataifa.
Wakati huo huo, Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Dk. Lihoya Chanwali, alisema kuanzishwa kwa Kampasi ya Tanga ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kusogeza huduma za elimu ya juu karibu na wananchi na kuongeza nafasi za udahili kwa wahitimu wa kidato cha sita.
Alisema kampasi hiyo iliyopo Kijiji cha Gombero, Wilaya ya Mkinga, itaanza kutoa programu mbalimbali kuanzia ngazi ya cheti, stashahada na shahada, huku ikitarajiwa kudahili wanafunzi wapatao 1,200 katika hatua za awali.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni miundombinu ya malazi, ambapo mabweni yaliyopo yana uwezo wa kuhudumia wanafunzi 360 pekee, na kuacha upungufu wa zaidi ya nafasi 900.
Kutokana na hali hiyo, Chuo Kikuu Mzumbe kimetoa wito kwa wawekezaji kujitokeza kuwekeza katika ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, nyumba za watumishi na huduma nyingine muhimu zitakazohitajika kadri kampasi inavyoendelea kukua.
“Iwapo tutapata wawekezaji watakaosaidia kujenga mabweni ndani au nje ya kampasi, tutakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi. Hii pia itachochea shughuli za kiuchumi katika Gombero na maeneo ya jirani,” alisema Dk. Chanwali.
Aliongeza kuwa kwa sasa chuo kina nyumba nne pekee za watumishi wakati mahitaji yanakadiriwa kuzidi nyumba 100 kutokana na matarajio ya kuwa na wafanyakazi zaidi ya 100 wa kada za kitaaluma na zisizo za kitaaluma.
Uongozi wa chuo unaamini kuwa uwepo wa Kampasi ya Mzumbe Tanga hautaongeza tu fursa za elimu ya juu, bali pia utakuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya ya Mkinga na Mkoa wa Tanga kwa ujumla kupitia ajira, biashara, uwekezaji na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma mbalimbali zinazotokana na uwepo wa taasisi kubwa ya elimu ya juu katika eneo hilo.
Ends .





