JAMII YATAKIWA KUSHIRIKIANA MALEZI YA VIJANA KUDUMISHA AMANI NA MAENDELEO

JAMII YATAKIWA KUSHIRIKIANA MALEZI YA VIJANA KUDUMISHA AMANI NA MAENDELEO

Na Hadija Bagasha, Tanga

Jamii imetakiwa kuendelea kushirikiana katika malezi na makuzi ya watoto pamoja na vijana ili kujenga kizazi chenye maadili mema, uzalendo na uwajibikaji kitakachokuwa chachu ya maendeleo na ustawi wa Taifa.

Wito huo umetolewa na Katibu wa Taasisi ya MIFTAH SALAAM, Idrisa Modo, wakati wa kongamano la amani lililowakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo, viongozi wa dini, vijana na wananchi kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha amani, mshikamano wa kijamii na maendeleo endelevu.

Akizungumza katika kongamano hilo, Modo alisema kuwa mafanikio ya taifa lolote huanza na malezi bora ya watoto na vijana, jambo ambalo linahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, viongozi wa dini, serikali pamoja na taasisi za maendeleo.

Alisema vijana ni rasilimali muhimu na nguvu kazi kubwa ya taifa, hivyo wanapaswa kupewa mwongozo sahihi utakaojenga maadili mema, nidhamu na moyo wa uwajibikaji ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.

“Malezi ya vijana si jukumu la wazazi pekee. Ni wajibu wa jamii nzima kuhakikisha tunawajenga katika misingi ya maadili, uzalendo na amani ili wawe viongozi bora wa kesho,” alisema Modo.

Aliongeza kuwa changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa, ikiwemo mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya vijana, zinaweza kudhibitiwa kupitia elimu sahihi, ushauri nasaha na ushirikishwaji wa vijana katika shughuli za kijamii na maendeleo.

Katika hatua nyingine, Modo alisema Taasisi ya MIFTAH SALAAM imejipanga kuufikia mkoa mzima wa Tanga kupitia programu mbalimbali za elimu, mafunzo na kampeni za uhamasishaji zinazolenga kukuza amani, mshikamano wa kijamii, maadili mema na maendeleo ya vijana.

Alieleza kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha ujumbe wa amani na maendeleo unawafikia wananchi wengi zaidi, hususan vijana ambao ni kundi muhimu katika ujenzi wa taifa.

Modo alisisitiza kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo kila mwananchi anapaswa kushiriki katika juhudi za kuilinda kwa kuwalea vijana katika misingi inayohimiza uvumilivu, mshikamano na kuheshimiana.

“Tunapowajenga vijana katika maadili mema na kuwapa fursa za kujitambua na kushiriki katika maendeleo, tunakuwa tumewekeza katika mustakabali salama wa taifa letu,” alisema.

Aidha, alitoa wito kwa wadau wa maendeleo, viongozi wa jamii na taasisi mbalimbali kuendelea kuwekeza katika programu zinazowajengea vijana uwezo wa kujitegemea na kuwa mabalozi wa amani katika maeneo yao.

Alisema kupitia ushirikiano huo, Tanzania itaendelea kujenga kizazi chenye maono, nidhamu na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi huku kikichangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya taifa.






Post a Comment

Previous Post Next Post

Contact Form