MBUNGE MONDULI ASISITIZA UMOJA NA MSHIKAMANO KATIKA JAMII YA KIMASAI
Na Joseph Ngilisho | Monduli
Mbunge wa Jimbo la Monduli, Isack Joseph Copriano, ameitaka jamii ya Kimasai kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano kama msingi wa kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na kulinda mila na desturi za jamii hiyo.
Mbunge huyo alitoa wito huo alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kumsimika Laigwanani Mkuu wa Jamii ya Maa Afrika Mashariki, Sinandei Makko, iliyofanyika Makuyuni, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.
Akizungumza mbele ya viongozi wa mila, wazee wa kimila na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Isack alisema kuwa umoja wa jamii ya Maa ni nguzo muhimu katika kujenga ustawi wa wananchi na kuhakikisha kuwa kizazi cha sasa na kijacho kinanufaika na fursa mbalimbali za maendeleo zinazopatikana nchini.
Alisema kuwa jamii ya wafugaji ina nafasi kubwa katika uchumi wa taifa, hivyo ni muhimu kuendelea kushirikiana, kuheshimu viongozi wa mila na kuendeleza utamaduni wao huku wakikumbatia elimu na maendeleo ya kisasa.
“Jamii yetu ya Kimasai imekuwa ikijulikana kwa mshikamano wake. Tunapaswa kuendelea kuuenzi umoja huo ili uwe chachu ya maendeleo, amani na ustawi wa wananchi wetu,” alisema mbunge huyo.
Katika hafla hiyo, Isack alimpongeza Laigwanani Mkuu mpya, Sinandei Makko, kwa kuaminiwa kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa kimila, akieleza kuwa jukumu lake ni muhimu katika kuimarisha mshikamano na kuunganisha jamii ya Maa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Alisema nafasi ya Laigwanani Mkuu ina heshima kubwa katika jamii ya Kimasai na ina wajibu wa kusimamia maadili, mila na desturi pamoja na kuhamasisha amani na ushirikiano miongoni mwa wananchi.
Kwa upande wake, Laigwanani Mkuu Sinandei Makko aliwashukuru viongozi wa kimila na wananchi wa jamii ya Maa kwa imani waliyoonyesha kwake, akiahidi kutumia nafasi hiyo kuendeleza umoja, kulinda utamaduni wa Kimasai na kushirikiana na viongozi mbalimbali katika kuleta maendeleo kwa jamii hiyo katika Afrika Mashariki.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa kimila kutoka maeneo mbalimbali ya jamii ya Maa, viongozi wa serikali, viongozi wa dini pamoja na mamia ya wananchi waliokusanyika kushuhudia tukio hilo muhimu la kihistoria kwa jamii ya Kimasai.
Ends

