MBUNGE MONDULI AWA MKALI KAMA PILIPILI APIGA MARUFUKU UUZAJI WA ARDHI ESILALEI, ATAKA MAENEO YA MALISHO YALINDWE KAMA MBONI YA JICHO

 MBUNGE MONDULI APIGA MARUFUKU UUZAJI WA ARDHI ESILALEI, ATAKA MAENEO YA MALISHO YALINDWE

Na Joseph Ngilisho – MONDULI

MBUNGE wa Jimbo la Monduli, Isack Joseph Copriano, amepiga marufuku shughuli zote za uuzaji wa ardhi katika Kata ya Esilalei baada ya kubainika kuwepo kwa madai ya watu wasiojulikana kuuza kinyemela eneo la malisho linalotumiwa na wananchi wa kijiji hicho.

Hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi, hususan wanawake zaidi ya 200 waliojitokeza kwa pamoja na kwenda katika eneo la Losirwa wakipinga hatua ya kuuzwa kwa eneo hilo, wakidai kuwa ni eneo muhimu kwa shughuli za malisho ya mifugo na ustawi wa jamii yao.

Wanawake hao walionekana wakipaza sauti zao huku wakiiomba serikali kuingilia kati haraka ili kuzuia kupotea kwa eneo hilo ambalo wamekuwa wakilitumia kwa miaka mingi kama sehemu ya malisho ya mifugo yao.

Akizungumza mbele ya wananchi hao wakati wa ziara yake katika eneo hilo, Mbunge Copriano alisema hataruhusu wananchi wa Monduli kuporwa maeneo yao muhimu kwa maslahi binafsi ya watu wachache, akisisitiza kuwa jukumu lake kubwa ni kutetea haki na maslahi ya wananchi wa jimbo lake.

Alisema tayari ameagiza Idara ya Ardhi ya Wilaya ya Monduli kufanya uhakiki wa haraka wa maeneo yote ya malisho yaliyopo katika Kata ya Esilalei ili kubaini uhalali wa umiliki wake na kuzuia migogoro zaidi ya ardhi.

“Mimi ni mwakilishi wa wananchi na nipo hapa kutetea maslahi yao. Hakuna mtu atakayechukua eneo la wananchi kiholela. Kesho nendeni mkaweke vibao vinavyoonesha wazi kuwa eneo hili ni la malisho na haliruhusiwi kuuzwa. Wananchi waogope matapeli wanaotaka kujinufaisha kwa kuuza ardhi ya kijiji,” alisema Mbunge huyo.

Aidha, Mbunge huyo alisisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kuhusika katika uuzaji haramu wa maeneo ya malisho au kuchochea migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa sasa wa kijiji hicho, Bwana Yamat, alikiri kulitambua eneo la Losirwa kama eneo rasmi la malisho na kuwataka wananchi kushirikiana kulinda ardhi yao dhidi ya watu wanaotaka kuuza maeneo ya kijiji kwa maslahi binafsi.

Alisema viongozi wa kijiji wataendelea kushirikiana na serikali ya wilaya kuhakikisha maeneo yote ya malisho yanatunzwa na kutumika kwa shughuli zilizokusudiwa ili kuondoa migogoro inayoweza kuhatarisha maisha ya wafugaji.

Wananchi waliohudhuria mkutano huo walimshukuru Mbunge huyo kwa kuitikia kilio chao kwa haraka, wakisema hatua yake imeleta matumaini mapya kwa jamii inayotegemea mifugo kama chanzo kikuu cha uchumi na maisha yao ya kila siku.

Katika ziara hiyo, Mbunge Copriano aliambatana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Kisioki Moitiko, pamoja na baadhi ya viongozi wa kata na kijiji waliofika kushuhudia mgogoro huo wa ardhi.







Ends..


Post a Comment

0 Comments