GAVANA TUTUBA ATOA ONYO KWA WAHASIBU, ATAKA TEKNOLOJIA NA UADILIFU KULINDA UCHUMI WA TAIFA
Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, ametoa onyo kali kwa wahasibu, wakaguzi wa hesabu na wataalamu wa fedha nchini akiwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kwenda sambamba na kasi ya teknolojia ili kulinda uchumi wa taifa dhidi ya ufujaji wa fedha, rushwa na mianya ya wizi wa kifedha.
Dkt. Tutuba alisema wataalamu wa fedha wana nafasi kubwa katika kuhakikisha mifumo ya fedha nchini inakuwa salama, yenye uwazi na inayoweza kufuatiliwa kwa urahisi kuanzia kwa mlipaji hadi kwa mpokeaji wa mwisho.
Akizungumza jijini Arusha wakati wa kongamano la wataalamu wa uhasibu, ukaguzi wa hesabu na washauri wa kifedha, Gavana huyo alisema dunia ya sasa imebadilika kwa kasi kubwa kutokana na maendeleo ya teknolojia, hivyo wataalamu wa fedha hawana budi kujibadilisha ili kuendana na mazingira mapya ya biashara na mifumo ya kifedha duniani.
“Tunataka kuona wahasibu na wakaguzi wa hesabu wanakuwa mstari wa mbele kuhakikisha miamala yote ya kifedha inafanyika kwa uwazi na usalama bila kuwepo mianya ya upotevu wa fedha,” alisema Dkt. Tutuba.
Alisema Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) tayari zimesaini makubaliano ya ushirikiano yatakayosaidia kuimarisha taaluma ya uhasibu, ukaguzi wa hesabu pamoja na usimamizi wa mifumo ya fedha nchini.
Katika hotuba yake, Dkt. Tutuba alisisitiza kuwa matumizi makubwa ya fedha taslimu bado ni hatari kwa wananchi na taasisi kutokana na uwezekano wa wizi, upotevu pamoja na matumizi yasiyo rasmi yanayoweza kuathiri uchumi wa taifa.
Alisema Benki Kuu inaendelea kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kufanya miamala ya kifedha kwa kuwa ni salama zaidi, rahisi kufuatilia na inapunguza mianya ya rushwa pamoja na ufujaji wa fedha.
“Leo hii kampuni za simu na taasisi mbalimbali zimeleta mifumo rahisi sana ya kutuma na kupokea fedha. Hakuna sababu ya kubeba fedha taslimu wakati teknolojia ipo na inaweza kusaidia kufanya miamala kwa usalama zaidi,” alisisitiza.
Aidha, alisema wataalamu wa fedha wanapaswa kuzingatia masuala ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi, utawala bora na uwajibikaji kwa kuwa dunia sasa inaelekea katika mifumo mipya ya ukaguzi na usimamizi wa fedha inayojumuisha tathmini za athari za kijamii na mazingira.
Kwa mujibu wa Gavana huyo, Tanzania inaendelea kufanya vizuri kiuchumi licha ya changamoto za kiuchumi zinazoikumba dunia, huku ukuaji wa uchumi ukiendelea kuwa wa wastani wa asilimia sita na mfumuko wa bei kubaki katika kiwango kinachodhibitika cha asilimia 3.3.
Alisema usimamizi mzuri wa fedha, matumizi ya teknolojia pamoja na uwajibikaji wa wataalamu wa sekta ya fedha vitasaidia Tanzania kufikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayolenga kukuza uchumi kufikia dola trilioni moja pamoja na kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja.
Dkt. Tutuba aliwataka wahasibu, wakaguzi wa hesabu na wataalamu wa fedha kuongeza ubunifu na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya fedha inaendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof.Siasa Mzenzi, alisema matumizi sahihi ya teknolojia pamoja na ushirikiano wa kitaaluma kati ya taasisi mbalimbali ni msingi muhimu katika kuimarisha sekta ya fedha nchini.
Profesa Mzenzi alisema kongamano hilo limewakutanisha wataalamu wa sekta ya fedha kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili masuala ya usimamizi wa fedha, matumizi ya teknolojia pamoja na utawala bora.
Alisema kongamano hilo limetokana na makubaliano ya ushirikiano kati ya NBAA na Benki Kuu ya Tanzania, ambapo taasisi hizo zimeamua kuunganisha utaalamu wao ili kuhakikisha mifumo ya kifedha nchini inaendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
“Sisi NBAA ni wataalamu wa masuala ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu, wakati Benki Kuu ni wataalamu wa masuala ya fedha. Tumeona ni muhimu kuunganisha nguvu na utaalamu wetu ili kuhakikisha mifumo yote ya kifedha inafuata misingi sahihi ya uwazi na uwajibikaji,” alisema Profesa Mzenzi.
Alibainisha kuwa kongamano hilo pia limejikita kujadili masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG), akisema dunia ya sasa inahitaji taasisi na mashirika kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia maendeleo endelevu.
Profesa Mzenzi alisema maendeleo ya teknolojia yanawataka wahasibu na wakaguzi wa hesabu kwenda sambamba na mabadiliko hayo ili kuendelea kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa na zinazokidhi mahitaji ya wakati wa sasa.
Aidha, alimshukuru Gavana wa Benki Kuu kwa kushiriki kufungua kongamano hilo, akisema hatua hiyo inaonesha namna serikali inavyotambua mchango wa taaluma ya uhasibu na ukaguzi katika kukuza uchumi wa taifa.
Ends..









0 Comments