ASILIMIA 70 YA WAGONJWA WA MOYO UKANDA WA KASKAZINI WASHINDWA KUFIKA JKCI, KCMC KUJENGA KITENGO MAALUMU CHA MOYO

 ASILIMIA 70 YA WAGONJWA WA MOYO UKANDA WA KASKAZINI WASHINDWA KUFIKA JKCI, KCMC KUJENGA KITENGO MAALUMU CHA MOYO

Na Hadija Bagasha, Tanga

Asilimia 70 ya wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kutoka Ukanda wa Kaskazini wamekuwa wakishindwa kupata huduma katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kutokana na changamoto za gharama kubwa za usafiri, malazi na maisha wanapolazimika kwenda Jijini Dar es Salaam kwa matibabu.

Kutokana na hali hiyo, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC imeanza ujenzi wa kitengo maalumu cha matibabu ya magonjwa ya moyo kinachotarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda JKCI.

Kitengo hicho kinatarajiwa kuhudumia kati ya asilimia 40 hadi 60 ya wagonjwa wa moyo kutoka mikoa ya Ukanda wa Kaskazini, hatua inayotajwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi waliokuwa wakikumbwa na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo za kibingwa.

Mahitaji ya huduma za matibabu ya moyo yameendelea kuongezeka nchini huku wananchi wengi wakishindwa kumudu gharama za safari na maisha ya Dar es Salaam, jambo linalosababisha baadhi yao kuchelewa kupata matibabu au kushindwa kabisa kufika hospitalini kwa wakati.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Tanga, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Batilda Burian amesema ujenzi wa kitengo hicho ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Ukanda wa Kaskazini.

Amesema Serikali pamoja na wadau mbalimbali wanaendelea na jitihada za kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma za matibabu ya moyo karibu na maeneo yao.

Balozi Dkt. Batilda amewataka wadau, wafanyabiashara, taasisi binafsi, mashirika pamoja na wananchi kujitokeza kuchangia fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo, huku lengo likiwa ni kukusanya zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vitakavyotumika katika hospitali hiyo.

“ Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa inayohudumiwa na Hospitali ya KCMC kama hospitali ya rufaa ya kanda. Uwepo wa kitengo hiki utaondoa adha kubwa kwa wananchi wetu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda Dar es Salaam kutafuta huduma za moyo,” amesema Batilda.

Kwa upande wake, Meneja wa Miradi na Afisa Mipango wa Hospitali ya KCMC ambaye pia ni Mratibu wa Ujenzi wa Kitengo cha Magonjwa ya Moyo, Emmanuel Bianchi amesema mradi huo tayari umefikia asilimia 40 ya utekelezaji wake.

Amesema gharama za mradi huo ni zaidi ya shilingi bilioni 25 ambapo tayari wamefanikiwa kupata zaidi ya shilingi bilioni 22 kutoka kwa wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi, huku kiasi kilichobaki kikihitajika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.

“Kimsingi huu ni mradi mkubwa unaolenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya za kibingwa na kibingwa bobezi hapa nchini. Tunataka kuhakikisha wananchi wa Ukanda wa Kaskazini wanapata huduma bora karibu yao bila kulazimika kwenda mbali,” amesema Bianchi.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa kitengo hicho kutasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda JKCI pamoja na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa matibabu ya moyo, hali ambayo imekuwa ikitumia fedha nyingi za Serikali na wananchi.

Aidha amesema wagonjwa wengi waliokuwa wakipewa rufaa kwenda Dar es Salaam wamekuwa wakikwama kutokana na gharama za usafiri, malazi na maisha ya kila siku, hali inayowafanya baadhi yao kushindwa kupata huduma kwa wakati.

“Huduma hizi kusogezwa karibu na wananchi ni hatua kubwa ya kuokoa maisha ya watu wengi pamoja na kupunguza mateso kwa familia ambazo zimekuwa zikigharamia safari za muda mrefu kutafuta matibabu,” ameongeza.

Ujenzi wa kitengo hicho cha kisasa cha matibabu ya moyo unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya afya inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo nchini, hususan kwa wananchi wa mikoa ya Kaskazini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitegemea huduma hizo kutoka Dar es Salaam pekee.



Post a Comment

0 Comments