MBUNGE LUKUMAY AIOMBA SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA UJERUMANI KUBORESHA HUDUMA ZA JAMII ARUMERU MAGHARIBI
Na Joseph Ngilisho|Arushadigital
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuona namna bora ya kuimarisha ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Serikali ya Ujerumani ili kusaidia uwekezaji katika sekta muhimu za kijamii zikiwemo afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara.
Dkt. Lukumay alitoa ombi hilo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, ambapo alimweleza dhamira na utayari wa wadau wa maendeleo kutoka Ujerumani kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha maisha ya wananchi wa Arumeru Magharibi kupitia miradi ya maendeleo.
Katika maelezo yake, Dkt. Lukumay alisema kabla ya kuingia rasmi katika siasa alikuwa akijihusisha na shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kushirikiana na taasisi na wadau kutoka Ujerumani, hususan katika kusaidia huduma za kijamii kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
Alisema uzoefu huo umeonyesha kuwa bado kuna haja kubwa ya kuimarisha uwekezaji katika huduma za msingi, hasa katika maeneo yanayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Arusha pamoja na Msitu wa Meru-USA, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za miundombinu na upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.
“Maeneo mengi ya wananchi wanaozunguka hifadhi hizi bado yanahitaji uwekezaji mkubwa katika maji safi na salama, elimu bora, vituo vya afya pamoja na barabara za kuunganisha vijiji na masoko. Ushirikiano wa kimataifa unaweza kuwa chachu kubwa ya maendeleo kwa wananchi wetu,” alisema Dkt. Lukumay.
Mbunge huyo alieleza kuwa baadhi ya kata na vijiji vinavyohitaji kupewa kipaumbele ni pamoja na Kata ya Oldonyowas katika vijiji vya Losinoni Chini, Losinoni Juu na Engutukoit; Kata ya Oldonyosambu yenye vijiji vya Oldonyosambu, Lemanda na Lemong’o; pamoja na Kata ya Olmotonyi inayojumuisha vijiji vya Olmotonyi, Ngaramtoni na Emaoi.
Maeneo mengine aliyoyataja ni Kata ya Kimunyak yenye vijiji vya Kimunyak na Olmuringaringa; Kata ya Kiutu katika kijiji cha Olgilai; Kata ya Sambasha yenye vijiji vya Timbolo na Sambasha; pamoja na Kata ya Olturoto katika kijiji cha Oldonyosapuk.
Aidha, Dkt. Lukumay alisema Kata ya Soon II katika kijiji cha Ng’iresi pamoja na Kata ya Bangata katika vijiji vya Midawe na Sasi ni miongoni mwa maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Kwa upande wa maeneo yanayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Arusha, mbunge huyo alitaja Kata ya Bangata katika vijiji vya Midawe na Sasi, Kata ya Oldonyowas katika vijiji vya Engutukoit na Lesinoni Juu, pamoja na Kata ya Oldonyosambu katika vijiji vya Lemong’o na Lemanda kuwa sehemu zinazostahili kupewa kipaumbele maalum kutokana na mazingira yake ya kipekee.
Alisema uwekezaji katika maeneo hayo utaongeza fursa za maendeleo kwa wananchi huku ukiimarisha pia uhifadhi wa mazingira kwa kuwasaidia wananchi kupata huduma bora na shughuli mbadala za kiuchumi.
Dkt. Lukumay alisisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa una nafasi kubwa katika kuharakisha maendeleo ya wananchi wa vijijini na kwamba Serikali ikiendelea kufungua milango kwa wawekezaji na washirika wa maendeleo, sekta za kijamii zitaendelea kuimarika kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake, Waziri Mahmoud Thabit Kombo aliahidi kuyafanyia kazi mapendekezo hayo kwa kushirikiana na wizara na taasisi husika ili kuhakikisha fursa za ushirikiano wa maendeleo zinazopatikana kupitia washirika wa kimataifa zinawanufaisha wananchi moja kwa moja, hasa wa maeneo ya vijijini.
**Ends**

إرسال تعليق