MAHAKAMA KUU YAMPIGA STOP MSAJILI WA VYAMA ALIYEPANIA KUIFUTA CHADEMA,YAZUIA HATUA YOYOTE KUJICHUKULIA

 MAHAKAMA KUU YAZUIA HATUA DHIDI YA CHADEMA, MSAJILI ASITOE FAINI KWA SASA

Na Arushadigital|Dar Es Salaam

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imepata nafuu ya muda baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Babati mkoani Manyara, kutoa amri ya muda inayomzuia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua hatua yoyote dhidi ya chama hicho, ikiwemo kukitoza faini au kuendelea na hatua za kinidhamu.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Irvin Mugeta wakati akisikiliza shauri la maombi ya Mapitio ya Kimahakama (Judicial Review) namba 12812 ya mwaka 2026 lililofunguliwa na Katibu Mkuu pamoja na Wadhamini Waliosajiliwa wa CHADEMA dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika uamuzi wake, Jaji Mugeta amesema maombi hayo yaliwasilishwa kwa dharura kufuatia hofu ya kuwepo kwa hatua zinazotarajiwa kuchukuliwa dhidi ya CHADEMA, hatua ambazo zingeweza kujumuisha kusimamishwa kwa usajili wa chama hicho au kutozwa adhabu ya kifedha kabla ya kusikilizwa kwa hoja za msingi za upande wa walalamikaji.

Mahakama imeelezwa kuwa viongozi wa CHADEMA walikuwa na wasiwasi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa huenda alikuwa tayari ameshafikia uamuzi kabla ya kutoa nafasi ya kusikiliza utetezi wao, jambo walilodai linakiuka misingi ya haki za asili na utawala wa sheria.

Akitoa maelezo yake, Jaji Mugeta alisema suala la iwapo kauli zinazodaiwa kutolewa na CHADEMA zina sifa za uchochezi au la ni jambo linalohitaji uchunguzi wa kina wa kisheria na haliwezi kuamuliwa kwa hatua ya awali bila kusikiliza pande zote zinazohusika.

“Mahakama imeamua kutoa amri ya muda inayomzuia Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua hatua yoyote dhidi ya CHADEMA hadi shauri hilo litakaposikilizwa na kuamuliwa baada ya kusikiliza hoja za pande zote,” amesema Jaji Mugeta katika uamuzi wake.

Uamuzi huo unaonekana kuongeza mvutano mpya wa kisiasa na kisheria kuhusu mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Siasa dhidi ya vyama vya upinzani, huku wadau mbalimbali wakisubiri kwa karibu mwenendo wa shauri hilo ambalo linaweza kuwa na athari kubwa katika taswira ya demokrasia na uhuru wa vyama vya siasa nchini.

Kwa sasa, CHADEMA itaendelea na shughuli zake kama kawaida hadi pale Mahakama itakapotoa uamuzi wa mwisho katika shauri hilo ambalo tarehe ya kusikilizwa kwake itatangazwa baadaye na Mahakama.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم