Kamati ya Elimu, Afya na Maji Yaibua Changamoto ya Ukosefu wa Chakula Mashuleni Longido
Na Joseph Ngilisho, LONGIDO
KAMATI ya Elimu, Afya na Maji ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido imeibua changamoto ya ukosefu wa chakula kwa wanafunzi mashuleni, hali inayotajwa kuchangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika baadhi ya shule za msingi wilayani humo.
Changamoto hiyo imebainishwa May 22,2026 wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya kamati hiyo katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Longido kilichowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Noondoto, Oberd Njipai.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Njipai alisema kamati imebaini kuwa shule nyingi zinazofanya vibaya katika matokeo ya mitihani zinakabiliwa na changamoto ya wanafunzi kutopata chakula cha mchana shuleni.
Alisema hali hiyo imekuwa ikiathiri mahudhurio ya wanafunzi, umakini darasani pamoja na maendeleo ya taaluma kwa ujumla.
Kutokana na hali hiyo, kamati imependekeza viongozi wa vijiji, wazazi na jamii kwa ujumla kushirikiana na shule kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa chakula cha mchana ili kuboresha mazingira ya ujifunzaji na kuongeza ufaulu.
Mbali na changamoto ya chakula mashuleni, kamati hiyo pia imeeleza kuwepo kwa upungufu mkubwa wa walimu katika baadhi ya shule za msingi ikiwemo Shule ya Msingi Mangula na Gelai Bomba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baadhi ya shule zina idadi kubwa ya wanafunzi inayozidi uwezo wa walimu waliopo hali inayosababisha ugumu katika utoaji wa elimu bora.
Kamati hiyo imeitaka Idara ya Elimu ya Awali na Msingi kuhakikisha walimu wa kujitolea wenye taaluma na sifa stahiki wanapatikana ili kusaidia kupunguza changamoto hiyo.
Aidha, kamati imeiagiza halmashauri kuainisha shule zenye upungufu wa madawati na kuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika ujenzi wa madawati ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Katika sekta ya afya, kamati hiyo imeitaka halmashauri kuhakikisha vituo vya afya na zahanati zilizokamilika zinaanza kutoa huduma kwa wananchi haraka iwezekanavyo.
Baadhi ya vituo vilivyotajwa ni pamoja na Zahanati za Engusero, Losikito na Lololo ambazo zimekamilika lakini bado hazijaanza kutoa huduma kikamilifu.
Wakati huo huo, kamati hiyo imeitaka halmashauri kushirikisha madiwani katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuongeza uwazi na ushirikiano.
Mwisho, Oberd Njipai aliomba Baraza la Madiwani kupokea taarifa hiyo pamoja na kuyapitisha mapendekezo yote yaliyowasilishwa kwa lengo la kuboresha huduma za elimu, afya na maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Longido.
Ends..





0 Comments