HALMASHAURI YA LONGIDO YATENGA MILIONI 180 KWA VIKUNDI,KUANZA KULIPA WIKI IJAYO
Na Joseph Ngilisho, LONGIDO
HALMASHAURI ya Wilaya ya Longido imetenga kiasi cha shilingi milioni 180 katika robo ya nne ya mwaka wa fedha kwa ajili ya kuwezesha vikundi mbalimbali vya wananchi, huku fedha hizo zikitarajiwa kuanza kuingizwa kwenye akaunti za vikundi kuanzia wiki ijayo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Grace Mghase, wakati akijibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido.Mghase alisema utoaji wa fedha hizo hautafanyika kwa mgawanyo sawa kwa kila kikundi au kata, bali utazingatia sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa kwa wanavikundi husika ili kuhakikisha fedha zinawanufaisha walengwa waliokusudiwa.
Katika hatua nyingine, halmashauri hiyo imeendelea kutekeleza mpango wa kusaidia wananchi walioathirika na majanga ya asili ikiwemo ukame na mafuriko, ambapo serikali imeelekeza kufanyika kwa utambuzi wa kaya na wananchi wanaostahili kupatiwa msaada kupitia programu maalum ya ustawi wa jamii.
Ilielezwa kuwa kwa Wilaya ya Longido, jumla ya kata 20 zinaendelea kufikiwa na huduma hiyo, huku wataalamu 28 wakisambazwa katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutambua wananchi wanaostahili na kuhakikisha wanapatiwa huduma zinazohitajika.
Akizungumza katika kikao hicho, Mratibu wa TASAF Wilaya ya Longido, Silas Simon, alisema kuanzia Julai mwaka huu awamu ya tatu ya programu za ruzuku kwa kaya duni itaanza rasmi sambamba na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya mazingira pamoja na miradi mingine ya kijamii inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Katika sekta ya afya, halmashauri hiyo imeendelea kukamilisha miradi mbalimbali ikiwemo nyumba ya watumishi wa afya katika Hospitali ya Hosinike, ambapo zaidi ya shilingi milioni tano zimetengwa kwa ajili ya hatua za mwisho za malipo na ujenzi.
Aidha, ujenzi wa nyumba ya madaktari katika eneo la Isokonoe unaendelea baada ya kupatikana kwa shilingi milioni 15 kupitia mradi wa Kabongo.
Mkandarasi tayari ameanza kazi za ukarabati na maboresho mbalimbali ikiwemo mifumo ya maji safi na maji taka, huku hatua zilizobaki zikiwa ni uwekaji wa vifaa vya mwisho ili jengo hilo lianze kutumika rasmi.
Kwa upande wao, Madiwani walioshiriki kikao hicho walieleza kuridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo na kuwataka watendaji kuhakikisha miradi iliyobaki inakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma bora zinazotarajiwa.
Ends


0 Comments